Select Menu

function googleTranslateEl

HABARI KIMATAIFA

HABARI KITAIFA

Performance

Cute

My Place

MICHEZO

Racing

Videos

Wakati picha za majengo yenye nyufa zikisambaa mitandaoni ikidaiwa ni ya hosteli mpya za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umekwenda kukagua ili kujiridhisha.

Majengo hayo yaliyojengwa na TBA kwa miezi minane yakielezwa kugharimu Sh10 bilioni yalizinduliwa Aprili 15,2017.

Ujenzi ulifanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kumaliza tatizo la malazi kwa wanafunzi wa UDSM.

 Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, jana alisema hata yeye ameziona picha hizo kwenye mitandao ya kijamii.

“Nimeziona na muda huu najiandaa kwenda huko kuangalia kama taarifa hizo ni za kweli,” al;isema Mwakalinga 

Picha hizo zilianza kusambaa jana jioni. Mwakalinga alisema huenda picha hizo ni za majengo mengine lakini zimehusishwa na hosteli hizo.

“Nitatoa taarifa baada ya kukagua majengo hayo kwa sasa siwezi kuzungumza hadi nitakapoona,” alisema.

Serikali imepanga kuajiri walimu 11,000 wa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha wa 2017/18.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo alisema katika mpango huo, walimu 7, 000 watakuwa wa shule za msingi na 4,000 wa sekondari.

“Hadi kufikia Desemba 31, walimu 2,700 watakuwa wameshaajiriwa,” alisema Jaffo

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati wa kurekodi kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kurushwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Jafo alisema ajira hizo zitapunguza upungufu wa walimu unaotokana na ongezeko la wanafunzi tangu Sera ya Elimu Bure ya Msingi ianze kutekelezwa.

Tangu mwaka jana, Serikali inatekeleza sera hiyo inayoligharimu Taifa zaidi ya Sh20 bilioni kila mwezi, huku idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi na wale wanaojiunga na za sekondari ikiongezeka kwa zaidi ya wanafunzi milioni moja.

Kuhusu miundombinu shuleni alisema kwamba Serikali imetenga zaidi ya Sh37 bilioni za ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari za umma 148.

Akifafanua, Jafo alisema zaidi ya Sh21 bilioni zimetumika kujenga mabweni 85 katika awamu ya kwanza ya mpango huo, huku awamu ya pili ya kujenga mabweni 65 iliyoanza kutekelezwa Agosti ikitarajiwa kugharimu Sh16 bilioni.

Kuhusu matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa, Waziri Jafo alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh246 bilioni kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa katika shule za umma.

“Theluthi moja ya fedha hizo, sawa na Sh82 bilioni zitatumika kukamilisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi,” alisema.

Waziri Jafo alisema kuwa Serikali imepanga kujenga vituo vya afya 172 kwa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Canada na wadau wengine kupitia mfuko wa pamoja wa kuendeleza Sekta ya Afya (Basket Fund).

“Lengo ni kutekeleza sera ya zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za afya,” alisema Jafo.

Alifafanua kuwa hivi sasa ni kata 530 pekee kati ya 3,900 zilizopo nchini ndizo zenye vituo vya afya.

Kuhusu upatikanaji wa dawa na vifaatiba, alisema Serikali imeongeza bajeti hadi kufikia Sh269 bilioni kwa ajili hiyo.

“Tunazo pia zaidi ya Sh127 bilioni za Basket Fund zitakazoelekezwa kwenye utatuzi wa changamoto ya upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma,” alisema.

Akizungumzia upungufu wa watumishi katika sekta ya afya iliyochangiwa na uhakiki wa vyeti feki, Waziri Jafo alisema tayari Serikali imeajiri watumishi 2,058 huku wengine zaidi wakitarajiwa kuajiriwa.

Suala la uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali mwaka jana liliwanasa zaidi ya watumishi 19, 000 ambao ajira zao zilisitishwa, huku sekta ya afya na elimu zikiathirika Zaidi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam ambapo alibaini uwepo wa makontena yenye magogo ambayo ni mazao ya misitu yaliyokaa bandarini hapo kwa zaidi ya miaka 10.

Waziri Kigwangalla ameagiza Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii atangaze kujitokeza kwa wamiliki wa magogo hayo 938  na kama wamiliki wasipojitokeza, magogo hayo yatakuwa mali ya Serikali.

Aidha Dkt. Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 yanayodaiwa kuingizwa nchini kutoka nchini Zambia kujitokeza na kuwasilisha nyaraka zao zenye kuthibitisha kama kweli yalivunwa nchini Zambia na yalivunwa wapi na kwa vibali gani vya nchi hiyo pamoja na kufuatilia nyaraka za kuingiza ndani ya Tanzania.

Ameagiza kitengo cha kuzuia ujangili kifuatilie kubaini uhalisia na uhalali wa taarifa hizo vinginevyo yatakuwa mali ya Serikali.

Dkt. Kigwangalla amefanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo kufuatia uwepo wa taarifa za uvunaji holela wa magogo nchini, ambapo kuna taarifa kuwa kuna wafanyabiashara wa kigeni wanagawa vifaa vya kuvunia bure kwa ahadi ya kuuziwa mzigo na wahusika, pia uwepo wa taarifa kwamba kuna baadhi ya watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanaotoa vibali na kugonga nembo kinyume cha taratibu za kisheria, hali inayotishia usalama wa raslimali adimu ya misitu yetu ya asili.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu wakifuatilia majadiliano na kuchangia hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa  baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) kuwasilisha Muswada huo kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
..............................................................................................

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuanzisha chombo cha kuendesha na kudhibiti sekta ndogo ya usafiri majini, usalama wa meli na mazingira ya bahari ili kulinda maslahi mapana ya taifa.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akijibu hoja ya Serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.

Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kupeleka Muswada Bungeni wa kutunga sheria ambayo itaanzisha Shirika  la Wakala wa Meli wa Taifa (NASAC)  ambao utasimamia usalama wa meli na bahari zetu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa bandari zetu kama mnavyojua bandarini kumekuwa na changamoto nyingi.

“Hivi karibuni tumeshuhudia upotevu wa mali na vitu vingi pale bandarini kama vile madini na vitu vingine vinaingia bila utaratibu,” amefafanua Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa Serikali imeona ibadilishe mtazamo uliokuwepo zamani kupitia SUMATRA ambayo inasimamia masuala ya nchi kavu na majini, “Serikali imeona ianzishe chombo kingine ili kiweze kujikita kusamimia masuala ya usafiri wa majini pekee na masuala nyeti hasa ya uchumi wetu kama vile madini”.

Chombo kimoja cha kutoa huduma na kudhibiti sio jambo geni. Hapa nchini tunayo taasisi ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) ambayo inatoa huduma ya anga na kudhibiti anga, hivyo Serikali inataka kufanya hivyo pia kwenye sekta ya usafiri wa majini.

Hili si jambo geni kwa kuwa linafanyika kwenye nchi nyingine kama vile ya bandari ya Singapore na nchi nyingine ya India.

Aidha, Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali kuanzisha chombo hiki. Pia amefafanua kuwa SUMATRA haitapokonywa majukumu yake bali nia ya Serikali ni kuitaka SUMATRA isimamie sekta ya nchi kavu tu kwa maana ya barabara, reli, magari ambayo ni sehemu kubwa na ina changamoto ambayo inahitajika kutatuliwa hivyo ijikite huko na sekta hii ndogo ya usafiri wa majini iwe na chombo kingine tofauti ili sheria iweze kutusaidia kukuza uchumi wa baharini na wa nchi kavu.

Ni imani ya Serikali kuwa, kwa kuwa na chombo cha udhabiti cha sekta ya nchi kavu ambapo NASAC itaanzishwa kwa ajili ya sekta ya usafiri wa majini, utaziwezesha sekta hizi za majini na nchi kavu kukua vizuri hivyo kukuza uchumi wetu, watanzania watapata ajira na kampuni nyingi za meli zitaingia nchini na kufanya kazi kwa kuwa mahali ambapo hakuna udhibiti sekta haiwezi kukua, “angalieni sekta nyingine kama ya mawasiliano ambako kuna udhibiti mzuri na sekta inakua vizuri” amesema Prof. Mbarawa.

Kwa mantiki hiyo, Serikali itawasilisha sheria ya SUMATRA Bungeni ili kufanyiwa maboresho ili iweze kuchangia vizuri ukuaji wa sekta ya nchi kavu na iende na wakati.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof.

Norman Sigalla King amesema kuwa azma ya Serikali ni nzuri katika muendelezo wa kuhakikisha kuwa taasisi zinazoanzishwa zina mgusa mlaji na kwa manufaa ya Serikali kwa ujumla. Serikali imejibu hoja zote za wadau na Kamati yetu inaendelea kuchambua hoja hizo ili kuhakikisha kuwa  inasimamia na kuishauri Serikali kwenye Muswada huu.

Ni dhamira ya Kamati kuona kuwa biashara bandarini inaendelea kuimarishwa na kudhibitiwa; na nchi yetu sio pekee yenye bandari kwenye ukanda huu hivyo ni lengo la Kamati kuhakikisha kuwa Muswada huu unaopendekezwa unaboreshwa ili kuhakikisha una akisi ushindani.

Ameongeza kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza udhibiti kwenye bandari yetu, hivyo huu ni mlolongo wa kusimamia na kudhibiti shughuli za uendeshaji wa bandari.

Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amewaomba Watanzania kukichangia Chama hicho ili kiweze kuwafikia na kuwaeleza mambo makuu mawili wakati wa mikutano ya kampeni ya udiwani.

ACT- Wazalendo imesimamisha wagombea 28 kati ya 43 katika uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika Novemba 26 ambapo kampeni zake zimeanza Oktoba 29.

“Nachukua fursa hii kuwaomba Watanzania wenye uchungu na nchi yetu kuchangia kampeni zetu. Tunataka kufika kila ya kona ya nchi yetu na wewe ndio utatuwezesha kufika,” amesema Zitto

“Chochote ulicho nacho tunaomba utuchangie kwa kutumia namba hizi hapa. Tigo pesa 0713957977 na M-Pesa 0744959112,  Asante Sana,” ameongeza

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini Chama hicho kitatumia kampeni hizo kuwaeleza  Watanzania mambo makuu mawili ambayo ameyataja kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wananchi na hali ngumu ya maisha ya wananchi.

“Lengo kubwa ni kuwaamsha Watanzania kukataa ubinywaji wa haki za binaadamu na kutaka mabadiliko ya sera za uchumi ili kuongeza ajira na kuondoa umasikini,” amesema Zitto

Amesema watatumia mifano halisi kwenye kata husika na kutoa sera mbadala kwa misingi ya Azimio la Tabora.

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amembeza aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu kwa kujivua uanachama wa chama hicho na kuonyesha dhamira ya kujiunga na Chadema.
 
Nape aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amekuwa mbunge wa pili wa CCM kuzungumzia uamuzi wa Nyalandu akitanguliwa na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ‘Kibajaji.’
 
Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Nape ameandika ujumbe ukiambatana na picha inayowaonyesha yeye, Nyalandu na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana wakiwa na nyuso za tabasamu.
 
Ujumbe huo ulisomeka “Chama cha siasa ni itikadi, itikadi ni imani, siamini sana katika kubadili imani kienyeji. Nitashughulikia mapungufu nikiwa ndani sio nje!”

Nape Moses Nnauye @Nnauye_Nape
Chama cha siasa ni ITIKADI, itikadi ni IMANI.Siamini SANA katika kubadili Imani KIENYEJI.Nitashughulikia MAPUNGUFU nikiwa ndani sio NJE!

Mwalimu Abasi Hussein wa shule ya msingi Mwabomba iliyopo tarafa ya Ngula wilayani Kwimba mkoani Mwanza anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kukutwa darasani akifanya mapenzi na mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye umri wa miaka 17.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mkoani humo na kusema mpaka sasa mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 27 anashikiliwa na jeshi la polisi muda wowote upelelezi ukikamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

"Babu wa mwanafunzi alipoona mjukuu wake amechelewa kurudi nyumbani alianza kufanya msako, alikwenda kwenye shule ya sekondari lakini hakumuona ikabidi aendelee kumtafuta mjukuu wake, ilipofika kwenye muda wa saa sita na kitu alikwenda kwenye shule ya msingi ya Mabomba katika moja ya darasa wakakuta huyo mwanafunzi wa kike akifanya mapenzi na  mwalimu wa shule hiyo ya msingi ya Mwabomba" alisema RPC Msangi

Msangi aliendelea kuelezea jinsi babu alivyoweza kuwakamata watu hao

"Yule babu alikuwa ameongozana na watu wengine hivyo walipowaona waliwakamata wakaita na watu wengine, baadaye taarifa zilifika kituo cha polisi na polisi walikwenda na kuwakuta watuhumiwa hao kwenye lile darasa hivyo wakawachukua na kuwafikisha kituoni, hivyo mtuhumiwa yupo kituo cha polisi tunaendelea na mahojiano na taratibu nyingine za kiupelelezi zinaendelea ili tuweze kukamilisha upelelezi tuweze kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo" alisisitiza Msangi

Mbali na hilo Kamanda Msangi ametoa onyo kwa watu wanaojihusisha na mapenzi na watoto chini ya miaka 17 na kusema huenda awe amekubali mwenyewe hilo ni kosa la ubakaji hivyo amewataka kuacha na kusema kufanya vitendo hivyo ni sawa na kuhitaji kwenda jela miaka 30.

Watu wawili wanaripotiwa kufariki wakati wakibatizwa siku ya Jumapili, kwenye mto ulio eneo la Rombo mkoa wa Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania.
Kwa mujibu wa naibu kamanda wa polisi Hamisi Selemani Issa, watu hao walikuwa wakibatizwa kwa kuzamishwa ndani ya maji, katika zoezi lililokuwa likiendeshwa na mhubiri wa Kanisa la Shalom huko Rombo.
Walizama maji katika mto Ungwasi wakati walikuwa wakizamishwa baada ya kile kinachotajwa kwa kulemewa na mawimbi makali ya mto huo.

  • Haijulikani ni kwa njia gani mhubiri na waumini wengine waliokuwa wakiendesha zoezi hilo walinusurika.
Polisi baadaye waliitwa kuondoa maiti baada ya ajali hiyo.
Naibu kamanda wa polisi aliiambia BBC kuwa waumini wa kanisa akiwemo pia mhubiri wamezuiliwa ili kuhojiwa.

Rais John Pombe Magufuli ameendelea kupongezwa na wananchi pamoja na Taasisi za kiraia mbalimbali kutokana na misimamo yake na kazi kubwa anayoifanya ya kupigania rasilimali za nchi, kwa masilahi ya wanyonge na masikini.

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti leo, Julai 17, 2017 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Masjid Ridhwaa, Alhaj Suleiman Seif Nassor na aliyekuwa mgombea wa CCM wa Ubunge Jimbo la Sengerema kupitia kura ya maoni, Laurence Mabawa.

Wakati akizungumza na wanahabari, Alhaj Nassor amesema bodi hiyo imemamua kumpongea Dkt. Magufuli kutokana na kazi nzuri anayofanya tangu alipoingia madarakani.

Kwa upande wake Mabawa, amesema licha ya kumpongeza Rais Magufuli, ameandaa kampeni kabambe inayojulikana kama ‘Magufuli Baki’ inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni kwenye mikoa yote nchini, ambapo kupitia mikutano wananchi wenye nia njema watamuomba rais abaki katika msimamo wake wa kuwatetea wanyonge na masikini.

“Kampeni ya Magufuli Baki itahusisha mikoa yote ya Tanzania kwa kuwafikia wananchi wakiwemo wanafunzi wa sekondari kwa kufanya mikutano yenye nia njema ya kumwomba Rais abaki kwenye msimamo wake, kampeni hii itawapa fursa wananchi kutoa maoni yao kuhusu utendaji kazi wake iwe kwa kupongeza au kukosoa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mabawa amelaani baadhi ya wanasiasa na wananchi wanaotoa lugha za maudhi na kejeli kwa watu wanaojitokeza hadharani kumpongeza Rais Magufuli na serikali yake.

“Niombe TCRA kuwachukulia hatua kali wote wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuwatolea maneno ya kejeli na kuudhi watu wanaojitokeza kumpongeza Rais,” amesema.
Pacha walioungana, Maria na Consolata wamejawa na furaha baada ya kufaulu mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa, Kusini magharibi mwa Tanzania.
Maria na Consolata, walio na umri wa miaka 19, wamefaulu kwa kupata daraja la pili katika masomo yao ya kidato cha sita na kuwa na matumaini kuwa ndoto yao ya kuwa walimu hapo baadaye inaelekea kutimia.
Maria na Consolata wameieleza BBC furaha yao:
"Tulipokea matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya mwisho huwezi kujiamini sana," ameeleza Consolata.
Mabinti hawa wangependa kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani humo.
  • Wameeleza sababu za kuchagua chuo kwenye mkoa wanaoishi tofauti na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao wangependa kubadili mazingira.
"Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu tulivyo hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni baridi, hali hii tumeizoea.''
Maria na Consolata wanaona kuwa, hakuna linaloshindikana iwapo wazazi watawajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu
"Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.''
Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ni miongoni mwa waombolezaji wa kifo cha Linah, mke wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kilichotokea juzi.

Kikwete amewasili msibani leo, Julai 17 saa sita mchana na kuweka saini kwenye kitabu cha maombolezo.

Kikwete amemfariji Dk Mwakyembe na kumtaka awe mvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

"Mwakyembe ni rafiki yangu wa siku nyingi, hata wakati mama anaumwa aliniambia na nilienda kumjulia hali alipokuwa Muhimbili, nimtake awe mvumilivu tunajua ana majonzi msiba huu ni wetu sote,"amesema.

Wengine waliofika kumfariji Dk Mwakyembe ni Jaji Mstaafu Damian Lubuva, ambaye pia alimjulia hali Linah wakati akiwa hospitali.

"Nimekuja kumpa pole Harrison, tunafahamiana muda mrefu na mkewe alipokuwa anaugua pale Muhimbili nilikuwa naenda kumtembelea lakini juzi nilivyokuwa kijijini ndiyo nimepata taarifa za mama yetu ametutoka. Ni msiba wetu sote tunaelewa majonzi yake, uchungu aliyokuwa nao yeye na familia yake lakini kifo kimeumbwa na Mwenyezi Mungu kinapotokea sote ni tunatakiwa tumshukuru Mwenyezi Mungu," amesema.

Wengine waliofika kumfariji Dk Mwakyembe ni Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji; Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi; Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga na viongozi wengine wa Serikali waliopo madarakani na wastaafu.

Mjumbe wa kamati ya mazishi, Andrew Magombano amesema mwili wa Linah utaagwa kesho baada ya ibada itakayofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kunduchi kuanzia saa nne asubuhi.

"Baada ya ibada tutaaga na saa saba kamili tutaelekea uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kwenda Mbeya," amesema Magombano.

Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imewaachisha kazi wafanyakazi 12 waliokuwa wamesimamishwa kwa mwaka mmoja sasa.

Wafanyakazi hao walisimamishwa kazi Julai 2016 kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi.

Taarifa ya NSSF iliyotolewa leo Alhamisi (Julai 13) kupitia vyombo vya habari walioachishwa kazi ni Yacob Kidula, aliyekuwa mkurugenzi wa mipango, uwekezaji na miradi.

Wengine na nafasi walizokuwa wakishikilia kwenye mabano ni Ludocick Mrosso (mkurugenzi wa fedha), Chiku Matessa (mkurugenzi wa rasilimali watu na utawala), Sadi Shemliwa (mkurugenzi wa udhibiti, hadhara na majanga), Pauline Mtunda (mkurugenzi wa ukaguzi wa hesabu za ndani).

Crescentius Magori (mkurugenzi  wa uendeshaji), Amina Abdallah (meneja utawala), Abdallah Mselli (meneja wa uwekezaji), Mhandisi John Ndazi (meneja miradi), Wakili Chedrick Komba (meneja kiongozi Mkoa wa Temeke) na Ramadhani Nassibu (meneja mkuu usalama).

Wakati diwani wa saba wa Chadema akijiuzulu jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema hata yeye kama angekuwa na moyo mwepesi na mpenda fedha, angekuwa ameshahama upinzani.

Mbowe alisema jana kwamba kuwa kiongozi wa upinzani awe mbunge, diwani, au mwenyekiti wa mtaa, kunahitaji roho ngumu na kwamba hiyo si kazi ya watu wenye kupenda fedha, bali ni ya maumivu, kudhalilishwa, kunyimwa ushirikiano, kufungwa wakati wowote na kunahitaji msimamo wa hali ya juu.

“Upinzani ni wito, wenye roho nyepesi hawawezi, kama ningekuwa napenda fedha, nina roho nyepesi, ningeshachukua hizo pesa na ningeshakimbia kabisa upinzani,” alisema.

Mbowe amesema hayo wakati chama hicho kikipitia misukosuko ya madiwani wake wa Mkoa wa Arusha kukihama na jana ilikuwa zamu ya Diwani wa Ambuleni, Arumeru, Japhet Jackson.

Diwani huyo aliwasilisha barua yake ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri jana mchana pia kama wenzake sita, akisema anamuunga mkono Rais John Magufuli.

Diwani wa karibuni kujiuzulu wa Ngobobo, Solomon Laizer pia wa wilaya hiyohiyo katika jimbo linaloongozwa na Joshua Nassari wa Chadema.

Akizungumza kwa simu jana, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema wanaowania nafasi za uongozi na viongozi wa Chadema wanahitaji kuwa na msimamo wa hali ya juu.

“Mara nyingi wanaowania nafasi kwa upande wa upinzani, ni wale waliokomaa, lakini katika uchaguzi uliopita, chama kilichopata watu wengi ni Chadema. Kutokana na mfumo huo wa kuwafungulia milango, wakaingia wengi, mbu, mende na mambo mengine,” alisema.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alidai kwamba kuondoka kwa madiwani hao wa Chadema kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa Serikali hasa wakuu wa wilaya ambao wanataka kumfurahisha Rais.

“Inashangaza kuona wote wanaojiuzulu wanatoa kauli moja ya kumsifu Magufuli, ina maana hawana sababu nyingine labda pengine Chadema kuna matatizo, sera zao mbovu, kuna hiki na hiki hakijakaa sawa,”alisema.

Aliongeza kuwa juhudi za kuwarubuni viongozi wa Chadema zipo katika majimbo yote ya Chadema na juhudi hizo zinapata nguvu zaidi mahali ambako kuna mkuu wa wilaya dhaifu ambaye anatumia nguvu za ziada.

Alisema wamebaini kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya ndiyo wanaotumiwa na wamewekwa kwa makusudi kwa ajili ya kuua upinzani nchini.

“DC anawahimiza wanachama na viongozi eti wapeleke barua za kujizulu kwake, kwa sababu ana jeuri ya mamlaka. Kisheria hana mamlaka ya kupokea barua ya kujiuzulu kwa mwanasiasa. Tumebaini hawa baadhi ya watendaji wanatumiwa na kuahidiwa makubwa endapo watawadhibiti wapinzani,” alisema.

Alisema walipata tetesi za kujiuzulu kwa madiwani hao lakini hawakutaka kuchukua uamuzi wa kuwafukuza kwani si vizuri kuishi kwa tetesi lakini kwa kuwa wameamua kuondoka anawatakia kila heri.

Alisema baadhi ya madiwani hao walionekana kwenye vikao vya CCM na kusema mtu anayezidiwa akili na kudanganywa kwa fedha hata akibaki katika chama hatakuwa na maana.

“Kuliko kubaki na watu wengi wanaopenda fedha, wanaohadaiwa kwa rushwa, bora tubaki watu wachache wenye maadili,” alisema.

Mbowe alisema, licha ya Serikali kuudhofisha upinzani, chama hicho kinaamini kuwa safari yake ni kama ya treni ya kwenda Kigoma ambayo wapo wanaopanda na wanaoshuka.

“Bado tunavuna maelfu ya wana CCM, alianza Edwin Mtei, lakini sasa tunazungumzia wanachama zaidi ya milioni sita. Muelewe kuwa upinzani haudhoofiki, bali unakua,” alisema.

Alisema wale waliodhani watapata ulaji kama wa fedha, ndiyo wanaokuwa wepesi kuondoka na kwenda kutafuta wanachokitaka.

“Tuna imani watabaki wachache wenye imani na nafasi za walioondoka zitachukuliwa na wengine walio bora zaidi,” alisema.

Kuhusu kuswekwa rumande kwa saa 48 kwa amri za wakuu wa wilaya, Mbowe alisema sheria za kumuweka ndani kiongozi zina masharti yake.

“Kuna utaratibu wa kufanya.DC sio polisi, anaweza kuagiza polisi, kamkamateni fulani kisha mumhoji na kisha afunguliwe mashtaka, lakini si kumuweka ndani kwa saa 48. Haya maagizo yote yanatolewa na ngazi za juu. Sisi sasa tunawashtaki hao Ma-DC wote na hata mimi nimemshtaki DC wa Hai, kwa kuharibu miradi yangu,” alisema.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amewahakikishia wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga kwamba Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo baada ya kukagua zoezi la usajili wa wafanyabiashara hao linaloendelea katika katika Ofisi za TRA wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo ameshuhudia idadi kubwa ya wafanyabiashara hao wakiwemo waendesha bodaboda, mamalishe na wauza bidhaa mbalimbali wakiendelea kujisajili ili wapate vitambulisho.

“Ndio maana tumeona tuweke utaratibu wa kuwaandikisha na tuwapatie vitambulisho hatimaye tuweke mpango maalumu wa kuwapatia maeneo rasmi ya kufanyiabiashara zenu badala ya kila siku kuwatumia askari mgambo kuwafukuza wakati mnatafuta riziki,” alisema Dkt. Mpango.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwawekea wafanyabiashara hao wadogo utaratibu mzuri ii waendelee kufanya kazi zao za kujenga familia na Taifa kwa ujumla bila bughudha kwa kuwa Serikali inathamini mchango wao katika uchumi na maendeleo ya nchi.

“Ni lazima ifike mahali kila mtanzania achoke na umasikini, na sisi Serikali yenu tufanyekazi ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi badala ya kuwakandamiza,” aliongeza Dkt. Mpango

Dkt. Mpango amesema nchi ya Sweden imeweka utaratibu mzuri wa masoko maalumu kwa ajili ya wamachinga wao kila siku za Jumamosi na Jumapili ambapo watu wengi hufika maeneo hayo kununua bidhaa hali inayoashiria kuwa suala la uwepo wa wafanyabiashara wadogo wadogo ni la nchi nyingi duniani.

“Nawasihi mkawaeleze Watanzania wengine na wafanyabiashara ndogo ndogo wenzenu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili wasajiliwe na kupewa vitambulisho vitakavyowasaidia kujulikana,” alisisitiza Dkt. Mpango

Amerejea kauli yake ya kuwapongeza Watanzania wote kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kujitokeza kwa wingi kulipa kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya majengo kwa kuwa kodi hizo zinaipa Serikali nguvu na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.

Mkiona barabara zinajengwa, tunaboresha huduma za afya kwa nunua dawa za kutosha, mjue kuwa kodi yenu hiyo kidogo kidogo mnayotoa ndiyo inayotumika kuwezesha mambo hayo kufanyika (makofi)” Alisisitiza Waziri huyo wa Fedha na Mipango

Dkt. Mpango ameahidi kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi na vitendeakazi katika kituo hicho cha uandikishaji ama usajili wa wafanyabishara wadogo wadogo kilichoko katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Ilala Jijini Dar es Salaam ili kufanikisha kazi hiyo.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wadogo wadogo hao wameipongeza Serikali kwa hatua waliyoichukua ya kuwatambua rasmi na kuwaingiza katika mfumo wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya nchi.

Wamemwomba Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango awafikishie salamu zao za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, kwamba wanamuunga mkono katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendelo na kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi pamoja na kujenga nidhamu ya watumishi wa umma na matunda yake yameanza kuonekana katika uwajibikaji.

Credit. Mpekuzihuru
MAZUNGUMZO ya kumaliza mzozo wa mchanga wenye madini (makinikia), baina ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kupitia mshirika wake, Acacia, yanaweza kuwa si tu magumu, bali yakachukua muda mrefu kupata suluhisho.

Mazingira hayo yanatokana na uzoefu wa kampuni hiyo katika historia ya kimataifa kuonyesha kwamba inatumia umakini wa hali ya juu kulinda maslahi yake pale panapotokea nafasi ya mazungumzo ya kutafuta suluhisho la jambo lolote linalohusiana na uwekezaji wake katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa kutambua changamoto mbalimbali za kiuwekezaji, kampuni hiyo ina bodi maalumu inayohusika na ushauri wa kimataifa ambayo inaundwa na watu wenye ubobezi katika maeneo mbalimbali, hasa ya kisiasa na jiografia.
MTANZANIA Jumamosi limechunguza mwenendo wa kampuni hiyo kuhusu aina ya makubaliano yake ya kiuwekezaji na mataifa mbalimbali na kubaini kuwa imekumbana na misukosuko mikubwa ya uwekezaji wa madini.
Ukiachilia mbali masuala ya makinikia, ambayo kwa sasa yanaipeleka kampuni hiyo kwenye meza moja ya mazungumzo na Serikali, masuala ya mivutano ya ardhi, uchafuzi wa mazingira na migogoro ya mikataba nayo imekuwa ni sehemu ya misukosuko inayoikumba kampuni hiyo katika baadhi ya mataifa ambako imewekeza.
Gazeti hili limebaini kuwa, miongoni mwa mataifa ambayo yanaweza kuchukuliwa kama mfano au Tanzania kujifunza na hata kutafuta mbinu mpya ni Dominica na Saudi Arabia, ambako zilipitia changamoto kama hizi za mikataba mibovu iliyosababisha nchi hizo kunyonywa hadi pale pande zote mbili zilipolazimika kuketi meza moja ya mazungumzo.
Itakumbukwa mapema wiki hii, Rais Dk. John Magufuli baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton, nchi hizo zilitajwa kwamba zilipita njia kama hii hii inayopitia Tanzania kwa sasa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kupitia vyombo vya habari vya kimataifa na  kwenye mtandao wa intaneti umebaini kuwa, hata ule mgogoro wake wa mkataba wa uchimbaji wa madini  na Taifa la Dominica lenye takribani watu milioni 10, mazungumzo ya kutafuta mapatano yalidumu kwa miezi minane.
Inaelezwa kuwa, Serikali ya Dominica iliipa mkataba Kampuni ya Barrick Gold Cooperation wa kuchimba madini kwa miaka 30 katika mgodi wa Pueblo Viejo, ambao ni moja ya migodi mikubwa ya dhahabu duniani.
Katika uwekezaji huo, Kampuni zote mbili ambazo zinatoka nchini Canada, Barrick Gold Cooperation ilimiliki asilimia 60 na Goldcorp asilimia 40.
Msingi wa mgogoro baina ya serikali ya nchi hiyo na Kampuni ya Barrick ni mkataba ambao ulielekeza kuwa nchi hiyo ingenufaika kwa asilimia tatu tu ya faida ya dhahabu inayochimbwa.
Vyombo vya habari nchini Dominica vinaeleza kuwa, vuguvugu la maandamano ya wananchi yasiyokuwa na ukomo ambayo yaliongozwa na asasi mbalimbali za kiraia yaliisukuma serikali ya nchi hiyo kwa kiasi kikubwa kuupitia upya mkataba wake na Kampuni ya Barrick.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo hivyo, baada ya serikali ya nchi hiyo kupitia mkataba upya wa Barrick, iliingia kwenye mazungumzo na kufikia mwafaka wa kulipwa asilimia 28 ya fedha zitokanazo na faida ya dhahabu iliyochimbwa.
Taarifa hizo na zile za Kampuni ya Barrick zinaeleza kuwa; Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 25 kutoka malipo yaliyokuwapo kwenye mkataba wa awali uliokuwa unapigiwa kelele na wananchi.
Tangazo la makubaliano hayo baina ya kampuni hiyo na Serikali ya Dominica ambalo lilitolewa na Barrick Mei 8 mwaka 2013, lilitanabahisha kuwa kusudio la makubaliano hayo ni kuwa na uchumi wenye kunufaisha pande zote mbili.
Katika kutafuta makubaliano hayo, Barrick walipendekeza masharti manne ambayo yalijenga msingi wa kupatikana kwa suluhisho.
Masharti hayo, kwanza ni kuondolewa kwa asilimia 10 ya kodi iliyowekwa kwenye mtaji wa awali wa uwekezaji kwa ajili ya kupata faida (NPI).
Pili, kuongezwa kwa muda ambao utaiwezesha serikali ya nchi hiyo kupitia kampuni yake ya Pueblo Viejo Dominicana Corporation (PVDC) kurejesha mtaji wake uliowekezwa.
Tatu, kusogezwa kwa muda wa kuanza makato mapya yatokanayo na faida (NPI).
Nne, kuwekwa punguzo la kiwango cha makato ya thamani.
Taarifa zinaeleza kuwa, baada ya serikali kukubaliana na mapendekezo hayo, Barrick nayo iliridhia mapendezo ya serikali kwa muktadha wa kuanza kulipa  kiwango cha juu cha kodi kilichopendekezwa.
Hata hivyo, ulipaji huo ulianza kufanyika kwa masharti ya kwamba kodi itapandishwa na kushushwa kwa kutegemea bei ya dhahabu kwenye soko.
Pia kiwango cha juu cha makato ya kodi ya dhahabu kitakuwa kinapitiwa na kupangwa upya kila baada ya miaka mitatu kuendana na asilimia 90 ya kodi iliyokuwa inalipwa awali kwenye Kampuni ya Serikali ya PVDC.
Makubaliano hayo yalikadiriwa kuweka usawa wa 50/50 wa mzunguko wa fedha ya madini kati ya Kampuni ya Serikali PVDC na Serikali yenyewe, kati ya mwaka 2013 hadi 2016.
Matokeo yake, Serikali ilitarajia kuvuna zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 2.2 katika kipindi ambacho bei ya dhahabu itakuwa inauzwa kwa dola za Kimarekani 1,600 kwa wakia moja (ounce) ambayo ni sawa na gramu 28.3.
Zaidi faida ya kiuchumi ya mabadiliko hayo yalitarajiwa kufika dola za Kimarekani bilioni 1.5.
Kwa ujumla msingi wa makubaliano mambo matatu yaliafikiwa. Kwanza ni kuongezwa kwa kodi ya mapato kwa asilimia 25, pili mrahaba safi wa makinikia kutozwa kwa asilimia 3.2 na tatu, jumla ya faida yote ya madini kutozwa kodi ya asilimia 28.75.
Mgodi wa Pueblo Vienjo una uhai wa miaka 25 na  una madini ya kiwango cha juu na cha chini ambapo kwa mwaka unachangia wastani wa wakia (ounces) 625,000 hadi 675,000 za dhahabu kwa Kampuni ya Barrick.

MKATABA NA SAUDI ARABIA
Taarifa ambazo gazeti hili limezikusanya kutoka katika vyombo vya habari vya Saud Arabia na Kampuni ya Barrick, zinaonyesha kuwa kampuni hiyo mwaka 2014 ililazimika kuingia mkataba wa makubaliano ya uwekezaji wa asilimia 50 kwa 50 na Serikali ya Saudi Arabia kupitia kampuni yake ya madini Ma’aden, kwa ajili ya kuchimba madini ya shaba kwenye mgodi wa Shaba wa Jabal Sayid.
Katika usimamizi au kujua vyote vinavyotoka kwenye uchimbaji huo, mkataba unaipa nafasi Saudi Arabia kusafirisha makinikia ya shaba kwa gharama ya chini.
Kupitia uwekezaji huo, jumla ya pauni milioni 100(kilogramu milioni 45.3) za makinikia ya shaba hupatikana kwa mwaka.
Si hilo tu, mwekezaji huyo mpya atalazimika kufuata misingi yote ya viwango vya maendeleo ya kijamii na kuendeleza kile kinachoitwa ‘Saudization’, yaani kuwaendeleza wazawa katika teknolojia ya uchimbaji madini.

Chini ya makubaliano hayo, pia ni lazima kampuni hiyo iweke asilimia fulani ya nafasi za kazi kwa wananchi wanaozunguka mradi huo na pia kutoa mafunzo maalumu ya utaalamu kwa makampuni ya ndani ya nchi.

Tanzania pia inaweza kuchota uzoefu huu ama kwenda mbali zaidi, hasa wakati ambapo nchi inataka kurekebisha mikataba yake ya madini ambapo inadaiwa nchi inaibiwa sana.

Pamoja na hayo, licha ya kuwa na uzoefu wa changamoto kama hizi katika maeneo inakowekeza,  hata hivyo uamuzi huu wa serikali ya Rais Magufuli umeonekana kuiumiza kichwa Kampuni ya Barrick na Acacia kwa ujumla.
Juzi katika kikao cha wanahisa ambacho kilifanyika kwa njia ya simu, kikiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, kimetoa mwelekeo wa kutaka kujipanga sawasawa kuanzia kwenye kuunda timu ambayo itakuja kufanya mazungumzo hapa nchini.
Miongoni mwa mikakati yao, Acacia imetaka kupata ripoti ya pili iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli mapema wiki hii.
Gordon aliwaambia wanahisa hao kuwa ripoti ya kwanza tayari wamekwishaipata na watahakikisha wanaipata ya pili kabla ya kuanza kwa mazungumzo.
Pamoja na hilo, Acacia wametaka kufahamu mapema timu ambayo itaongozwa na Rais Magufuli katika mazungumzo hayo pamoja na namna mazungumzo yatakavyofanyika.
Katika kikao hicho, Ofisa huyo alikuwa makini kueleza moja kwa moja kama wamekubaliana kutekeleza na kile ambacho kimedaiwa katika ripoti hiyo, ikiwamo suala la ujenzi wa kinu cha uchenjuaji wa dhahabu, akisema kuwa suala hilo wameliacha kwenye mazungumzo pindi majadiliano yatakapoanza.

UCHUNGUZI WA TANZANIA KUHUSU MAKINIKIA
Machi mwaka huu serikali ilizuia makontena zaidi ya 200 kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuchunguza mchanga wa madini (makinikia) ambao ulikuwa unasafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjuliwa.
Mchanga huo ulikuwa ni mali ya Kampuni ya Acacia, ambayo ni kampuni mshirika wa Barrick Gold Corporation.
Baada ya zuio la mchanga huo, Rais Dk. John Magufuli aliteua kamati mbili kwa ajili ya kuchunguza makinikia hayo, ambapo kamati ya kwanza iliyokuwa inaundwa na wanasayansi ilibaini kiasi kikubwa cha madini ambayo yangeibiwa kupitia mchanga huo.
Kamati ya pili ya uchunguzi iliundwa na wachumi na wanasheria ambapo ilibaini zaidi ya Sh trilioni 100 zimeibiwa kupitia usafirishaji wa makinikia, huku sheria nyingi za madini zikikutwa na kasoro inayotoa upenyo wa wawekezaji kutorosha madini.
Baada ya ripoti ya pili ya wachumi na wanasheria kuwasilishwa, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, wakiwa na hisa asilimia 64, Profesa John Thornton, alikuja nchini na kukutana na Rais, Dk. John Magufuli, ambapo walifanya mazungumzo na kukubaliana kuunda timu mbili za majadiliano.
Timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick kutoka Canada na Marekani na watafanya majadiliano ambayo yatahusu namna ya kufikia mwafaka katika suala la kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi kwa faida ya pande zote mbili.
Na EVANS MAGEGE- MTANZANIA