KABLA ya ‘pambano la michuano’ kati ya wenyeji wa michuano ya Copa America 2016, Marekani vs Argentina Alfajiri ya kuamkia siku ya kesho, wachezaji mastaa kama Leonel Messi, Gonzalo Higuaini, Alexis Sanchez, Philippe Coutinho, Clint Dempsey, James Rodriguez, Arturo Vidal, Sergio Aguero, Angel Di Maria, Carlos Bacca, Javier Hernandez wamefanikiwa kutikisha nyavu katika game 28 zilizokwishachezwa katika michuano hiyo ya kuazimisha miaka 100 ya uhai wa Shirikisho la soka la Marekani ya Kusini.
Katika game 28 za michuano ya COPA jumla ya magoli 84 yamefungwa (wastani wa magoli 3 kwa kila mechi).
Hii inamaanisha licha ya uwepo wa makipa mahiri wa klabu kubwa za Ulaya katika michuano lakini bado ‘washambuliaji wana njaa ya mabao.’
Eduardo Vargas alifanya ‘maajabu ya michuano kihistoria’ baada ya kuzamisha magoli manne peke yake wakati mabingwa watetezi Chile walipoweka rekodi ya kuichapa 7-0 Mexico katika mchezo wa robo fainali ya mwisho.
Vargas alifunga mara mbili wakati Chile ilipolazimika kuifunga Panama katika game ya mwisho ya makundi ili kufuzu kwa robo fainali.
Magoli mawili ya Vargas katika ushindi wa 4-2 yalikuwa ya kwanza kwake katika michuano na mchezo uliofuata dhidi ya Mexico akatengeneza rekodi yake mwenyewe kimataifa na rekodi ya michuano. Sasa anaongoza chati ya wafungaji bora akiwa ameweka kambani magoli 6, yote akifunga katika game mbili zilizopita.
Wakati Claudio Bravo akiwa ameshaenda nyavuni kwake mara tano katika game nne za Chile, Sergio Romero naye ameshapelekwa mara mbili akiwa na mastaa wenzake wa Argentina.
Patrick Pemberton Wa Costa Rica ameondoka katika michuano akiwa ameruhusu magoli 6 katika mechi 3. David Ospina wa Colombia ameruhusu magoli manne katika game nne huku timu yake ikisubiri game ya nusu fainali dhidi ya Chile.
Nimewataja makipa hawa wanne kutoka vilabu vya Manchester United, Arsenal, FC Barcelona si kwa sababu ya majina yao makubwa, bali nataka nikuoneshe ni kwa namna gani makipa wa timu zote walivyo katika presha.
Marekani wameruhusu magoli matatu kwa maana hiyo timu nne ambazo zitacheza nusu fainali kiujumla zimeruhusu magoli 14 katika game nne nne.
Ni mechi tatu tu zimemalizika pasipo nyavu kutikiswa. Peru 0-0 Colombia (game ya robo fainali-Colombia walishinda kwa penalti 2-4), Brazil 0-0 Ecuador (game ya hatua ya makundi) na Costa Rica 0-0 Paraguay.
Kwa maana hiyo game 25 zilikuwa na magoli. Ubunifu ni mkubwa mno kwa wachezaji wa nafasi za kiungo na umaliziaji umekuwa wa kiwango cha uhakika kwa washambuliaji. Kinachoendelea Marekani na kile kinachopewa sifa katika Euro 2016 pale Ufaransa ni vitu viwili tofauti.
‘Raha ya mechi bao/magoli’ na kitu ‘kinacho-boa’ katika Euro ni uhaba wa magoli. Gareth Bale amemudu kufunga katika mchezo na kuisaidia Wales kumaliza kama vinara wa kundi la pili (B) juu ya England.
Cristiano Ronaldo yeye binafsi ‘amekwama’ na kama kiongozi wa Ureno anapaswa kuhakikisha magoli yanafungwa katika game yao ya mwisho dhidi ya Hungary siku ya kesho. Vinginevyo Ureno itatupwa nje ya michuano.
Goli la Luis Nani katika sare ya 1-1 dhidi ya Iceland ndiyo pekee lililofungwa na Ureno ambayo imejaza mastaa kama Ricardo Quaresma, Joao Moutinho, CR7, Nani, Ricky Calvalho, Pepe. Walishindwa kufunga dhidi ya Austria. Croatia na Spain timu ambazo zimejaza wachezaji wabunifu zaidi katikati ya uwanja kiujumla zimefunga magoli 7 katika game mbilimbili na zitakutana katika game ya mwisho ya kundi D.
Wenyeji wa michuano Ufaransa wamefunga magoli manne katika game 3 za makundi, Uswisi ambao pia wamefuzu kwa hatua ya 16 kutoka kundi A, wamefunga magoli mawili tu. England wamefunga magoli manne wakati Wales hadi sasa ndiyo timu iliyofunga magoli mengi zaidi katika michuano-magoli 6.
Katika game mbili, Ujerumani wamefunga magoli mawili tu, Poland ambayo inashika nafasi ya pili nyuma ya Ujerumani katika kundi C imefunga goli moja tu. Italia wamefunga magoli matatu katika game mbili, sawa na Ubelgiji.
Katika michezo 28 iliyokwisha chezwa katika orodha ya wafungaji hakuna jina la C.Ronaldo, Mario Gomes, Thomas Mueller, Roberto Lewandowski, Wayne Rooney, Harry Kane, Zlatan Ibrahimovic.
Kiwango cha juu kiubunifu kwa timu ya Wales kimewafanya kuwa na moto mkali, na utulivu, maarifa binafsi katika upigaji wa mipira iliyokufa kumemsaidia sana Bale kuwa kinara wa magoli. Katika michezo 28 (kabla ya game za usiku wa leo) ni magoli 51 yamefungwa (wastani wa 1.82 kwa kila game.)
Na kwa idadi ya game 28 zilizochezwa hadi sasa katika COPA (kabla ya game za nusu fainali) ni dhahiri ‘Mpira unachezwa Amerika, Ulaya hawana ubunifu.’ Makipa wanateswa Marekani, washambuliaji wamedoda Ufaransa.
Credited by: Baraka Mbolembole
No comments
Post a Comment