Kiongozi wa Nigeria Muhammadu Buhari amelalamika kwamba taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika limekuwa maskini ghafla.
Amesema hayo siku moja tu baada ya Afrika Kusini kutwaa tena nafasi ya taifa lenye uchumi mkubwa barani Afrika.
Nigeria ilikuwa imeshikilia nafasi hiyo kwa miaka miwili baada ya kutathmini upya uchumi wake.
Afrika Kusini iliipita Nigeria baada ya kutumiwa kwa viwango vya sasa vya ubadilishanaji wa fedha dhidi ya dola ya Marekani.
Sarafu ya rand ya Afrika Kusini imeimarika pakubwa ilhali naira ya Nigeria imeshuka sana.
Kwa sasa, thamani ya uchumi wa Afrika Kusini ni $301bn (£232bn) nao uchumi wa Nigeria $296bn.
Mataifa yote mawili hata hivyo si thabiti kiuchumi.
Akiongea mjini Abuja, Bw Buhari alisema: "Umekuwa mwaka mgumu sana kwa Nigeria. Kabla yetu kuingia madarakani, mafuta yaliuzwa $100 (£77) kwa pipa. Bei hii ilishuka hadi $37, na sasa ni kati ya $40 na $45 kwa pipa."
"Ghafla, tumekuwa taifa maskini, lakini kujitolea kwetu kuhakikisha uwazi na uwajibikaji kunazuia wananchi kuhisi kwamba kuna upungufu mkubwa katika uchumi."
Bw Buhari alichukua mamlaka mwaka jana baada ya kushinda uchaguzi wa urais.
Aliahidi kukabiliana na ufisadi na kuinua uchumi wa Nigeria.
No comments
Post a Comment