Na John Banda
Mkoa wa Dodoma umeanza rasmi kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli lililotaka kufanyika kwa usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya nchi siku ya tarehe 9 Disemba, 2015 kama mojawapo ya maadhimisho ya siku ya uhuru na kuwataka viongozi na wataalamu kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.
Uongozi wa Mkoa umeamua kuanza
mapema zoezi la ufanyaji usafi pasipo kusubiri tarehe 9 Disemba na umepanga
kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu likihusisha usafi wa kila siku na usafi wa
siku zote za Jumamosi kuanzia saa 1:00 hadi saa 3:00 asubuhi.
Taasisi mbalimbali zilizopo
Mkoani Dodoma zimetumia Jumamosi ya leo Novemba 28, 2015 kushirikiana na
wananchi kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma ambapo
Viongozi na Watumishi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Tume ya
Maendeleo ya Ushirika na Manispaa ya Dodoma wamefanya usafi eneo la Bahi Road
kuelekea Nkuhungu kwa kuondoa taka na michanga kwenye mitaro ya maji ya mvua,
kufyeka na kuchoma taka eneo la makaburi ya Kizota.
Kwa mujibu wa Ratiba ya usafi
iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Mamlaka ya majisafi na usafi
wa Mazingira mjini Dodoma-DUWASA ilifanya usafi eneo la kuanzia ofisi za waziri
mkuu (Mtaa wa Mahakamani) hadi ofisi za
hazina ndogo.
TANESCO Mkoa wa Dodoma
walisafisha eneo la kituo cha kuuzia mafuta cha BP Capital hadi soko la
Sabasaba.
Taasisi nyingine ni pamoja na jeshi la Magereza ambapo lilifanya
usafi kuanzia mzunguko wa barabara ya kuelekea Bahi hadi maeneo ya magorofa
mengi wakati mabenki yalisafisha mitaa na barabara zinazopita mbele ya majengo
yao ya benki na Wakala wa Barabara TANROADS wao walisafisha kuanzia kituo cha
mabasi ya mikoani hadi soko la Sarafina.
No comments
Post a Comment