Rais wa TFF Jamal Malinzi leo alikua na kikao cha pamoja na wajumbe wengine kutoka ZFA na TFF kuhusu hatma ya ushiriki wa Zanzibar katika mashindano ya kimataifa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Shirikisho la Soka Afrika CAF kuwa na mpango wa kutaka kulifungia shirikisho la soka Zanzibar kushiriki shughuli za mpira wa miguu duniani kutokana na kupeleka masuala ya mpira mahakamani.
Malinzi amesema baada ya kutambua uzito wa suala hilo ambalo lingeweza kupelekea Zanzibar kukosa ushiriki michuano ya CAF na CECAFA ili kunusuru soka la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wamefikia makubaliano mbalimbali ikiwemo kuitishwa mkutano mkuu wa ZFA wa dharura kujadili mwenendo wa kamati ya utendaji, mapato na matumizi ya ZFA pamoja na kuteua kamati ndogo ya kuandika upya Katiba ya ZFA chini ya Rais wa ZFA, Ravia Idarus.
Pia kamati ya sasa inayoendesha ligi Zanzibar, itaongezewa wajumbe watatu watakoteuliwa na Rais wa ZFA ili maamuzi yao yaweze kuwa na nguvu za kisheria na kikatiba, pia kikao kimeazimia kuwa mashauri yote yaondolewe Mahakamani na waliohusika kufungua mashtaka hayo wamekubali kuyaondoa mara moja.
No comments
Post a Comment