MWANAFUNZI
wa darasa la tano wa Shule ya Msingi Sekei iliyopo jijini Arusha, Cliff
Laiza (12) amekufa wakati akiogelea kwenye bwawa lenye kina kirefu
katika Hoteli ya Kitalii ya Mount Meru iliyopo jijini hapa katika
sherehe ya Krismasi.
\
Tukio hilo ni la juzi majira ya saa 12 jioni wakati Cliff na watoto
wengine, walipokuwa wakiogelea katika hoteli hiyo, ikiwa ni sehemu ya
kusherehekea Krismasi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Meneja wa Hoteli
ya Mount Meru , alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na
kusema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi na watatoa ufafanuzi baada
ya polisi kukamilisha upelelezi wa tukio hilo.
Baadhi ya watoto waliokuwa wakiogelea na Cliff kwenye hoteli hiyo,
walisema alihama ghafla kwenye bwawa la watoto na kwenda kuogelea bwawa
linalotumiwa na watu wazima, ambalo wakati huo hapakuwa na mtu yeyote
akiogelea, lakini ghafla hakuonekana tena hadi alipokutwa anaelea juu ya
maji.
Babu wa mtoto huyo, Emanuel Meage alieleza kusikitishwa na tukio hilo na
kueleza kuwa mjukuu wake aliaga kuwa anaenda kuogelea katika Hoteli ya
Mount Meru yeye na wenzake. Hata hivyo, alisema alishangaa kusikia
amekufa na kwa sasa wanamsubiri baba yake ili kujua ni hatua zipi
wanazichukua kutokana na tukio hilo.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wazazi waliutupia lawama uongozi wa
hoteli hiyo kwa kushindwa kuwa na usimamizi mzuri na ulinzi wa watoto
hao, badala yake wamekuwa wakijali kukusanya fedha na kuwaacha watoto
wajiongoze, hatua ambayo si sahihi kwa vile eneo hilo ni hatari na si
salama kwa mazingira ya watoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha tukio
hilo na kueleza kuwa polisi wapo kwenye uchunguzi na atalitolea
ufafanuzi baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema hakuna mtu anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
Chanzo-Habarileo
No comments
Post a Comment