Kama
tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi
wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu
kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa
wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.
Dawa
za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo tu
hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa. Bei
ya kununulia dawa hizi ni kati ya dola za kimarekani 55 hadi 85 (yaani
shilingi za kiTanzania 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo (vial)
kimoja. Kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu
baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi
mmoja tu.
Pamoja
na changamoto hizo, Serikali kupitia MSD kila mwaka huagiza dawa hizi
kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo
bei ya kuinunua kutoka MSD ni TZS 200,000/= kwa kichupa kimoja.
Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa
washitiri wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika
wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika.
Napenda
kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za
tiba hutolewa bure kwa makundi maalum, au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya
gharama, au kwa kupitia mfumo wa Bima mbalimbali za Afya kama vile CHF.
Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu
wa msamaha hutumika.
Katika
kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka
wanahudumiwa ipasavyo, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anatoa maelekezo yafuatayo:-
Waganga
Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Hospitali zote nchini wahakikishe kuwa
Hospitali zote za umma zinaingiza dawa hii katika dawa za dharura ili
iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia kifungu cha fedha
za dawa za dharura.
Kwa
wagonjwa ambao watakuwa na Bima ya Afya, basi gharama za matibabu hayo
zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa Bima. Wananchi wanahimizwa
kujiunga na Bima za Afya (CHF/NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya
na mengine. Mfano CHF - gharama ya kujiunga katika Halmashauri
mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000/= hadi shilingi 30,000/=
kwa mwaka.
Kwa
wagonjwa ambao watakuwa hawana Bima ya Afya, hao watatakiwa kuchangia
gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango
kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri
itavyohitajika.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba kung'atwa na nyoka ni ajali na wananchi
wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi
uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya
nyoka ni mdogo.
Wagonjwa
watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo, basi
hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za afya
wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa
msamaha wa gharama hizo.
Aidha,
kwa kuwa nchi yetu ni kubwa na ina nyoka wengi, Mhe Waziri wa Afya
anawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kupitia kwa
uangalifu takwimu za wagonjwa walioumwa na nyoka katika kipindi cha
kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na kuziwasilisha Wizarani kabla ya tarehe
31 Januari 2017 ili kupata takwimu za mahitaji halisi ya dawa ya sumu
ya nyoka nchini. Hii itasaidia kuboresha upangaji, uagizaji na
upatikanaji wa dawa hizo nchini.
Vile
vile, Waziri wa Afya ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuweka utaratibu
wa haraka wa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili
kupata unafuu wa bei.
Imetolewa na:-
Nsachris Mwamwaja
Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Afya
26/12/2016
No comments
Post a Comment