Ufaransa imetangaza hali ya hatari
na kufunga mipaka yake baada ya watu zaidi ya 120 kuuawa kwenye
mashambulio kadha mjini Paris.
Watu wenye silaha walishika mateka watu waliokuwa kwenye ukumbi huo kabla yao kuzidiwa nguvu na maafisa wa polisi.
Watu wengine waliuawa kwenye mlipuko uliotokea karibu na uwanja wa michezo wa taifa wa Stade de France ambako mechi ya kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani ilikuwa ikiendelea.
Wasimamizi wa mji wa Paris wamewataka raia kusalia manyumbani na wanajeshi 1,500 wametumwa kushika doria Paris.
Shambulio mbaya zaidi linaonekana kuwa hilo la Bataclan, ambako ripoti zinasema watu waliokuwa wamehudhuria tamasha ukumbini walipigwa risasi na kuuawa baada ya kushikwa mateka.
Akiongea baada ya kufika katika ukumbi huo baadaye, Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameapa kuwa wahusika watakabiliwa "bila huruma".
Mashambulio mengine yalitokea karibu na mighahawa ya Le Petit Cambodge na Le Carillon katika mtaa nambari 10 ambako mwandishi wa BBC anasema aliona watu 10 wakiwa wamelala chini, wakiwa wamejeruhiwa vibaya na wengine kufariki
Mtu aliyeshuhudia ameambia gazeti la Liberation kwamba naye alisikia risasi zaidi ya 100 zikifyatuliwa katika mghahawa wa La Belle Equipe katika mtaa nambari 11.
Milio ya risasi pia ilisikika katika kituo cha kibiashara cha Les Halles.
Rais wa Marekani Barack Obama amelitaja shambulio hilo kuwa "jaribio lisilokubalika la kuhangaisha raia wasio na hatia" na kuahidi kusaidia Ufaransa kukabiliana na waliohusika.
"Hili si shambulio tu dhidi ya raia wa Ufaransa. Ni shambulio dhidi ya binadamu wote na maadili yetu ya pamoja," amesema.
"Tutafanya kila tuwezalo kuwasaidia watu wa Ufaransa na mataifa kote duniani kuhakikisha magaidi hawa wanakabiliwa.”
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema ameshtushwa sana na shambulio hilo na kuahidi kufanya "lolote tunaloweza kufanya kusaidia."
NA BAADHI YA VIONGOZI WA DUNIA WAMETOA SALAMU ZA POLE KWA UFARANSA
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alitisha mkutano maalum wa dharura wa baraza la mawaziri, ujulikanao kama Cobra, Downing Street kufuatia mashambulio nchini Ufaransa. Awali, alieleza kushtushwa kwake na mashambulio hayo yaliyoua watu zaidi ya 120.
Viongozi mbalimbali wameendelea kutoa risala zao
Waziri mkuu mpya wa Canada Justin Trudeau amesema wako pamoja na “binamu zetu Wafaransa wakati huu wa giza na majonzi”. Ameahidi kuisaidia serikali ya Ufaransa.
Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ameshtushwa sana na “habari na picha zinazotufikia kutoka Paris”. Amesema anaomboleza na waathiriwa wa “linalodhihirika kuwa shambulio la kigaidi”.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameshutumu mashambulio yaliyotekelezwa mjini Paris.
Msemaji wa UN Stephane Dujarric amesema Ban ''anaamini Ufaransa ina uwezo wa kuwakamata na kuwatendea haki wahusika upesi."
Rais wa Iran Hassan Rouhani, aliyepangiwa kuzuru mji wa Roma na kisha Paris wikendi hii, ameahirisha ziara yake kutokana na mashambulio Paris.
Maafisa wa polisi wakisaidiana na wanajeshi wanashika doria maeneo mengi Paris baada ya watu 120 kuuawa katika mashambulio sita mjini humo. Hapa ni afisa wa polisi karibu na hospitali ya Saint Antoine mjini humo.
Raia wawili wa Sweden huenda wakawa miongoni mwa waathiriwa wa mashambulio Paris, wizara ya mashauri ya kigeni nchini humo imesema. Msemaji wa wizara hiyo Johan Tegel amesema wana habari raia mmoja wa Sweden amejeruhiwa na mwingine kuuawa.
Washambuliaji wanane wamefariki, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP. Saba walijilipua, na mmoja akauawa. Wanne walifariki katika ukumbi wa Bataclan, watatu kwa kujilipua na mmoja akauawa na polisi.
Watatu walifariki karibu na uwanja wa michezo wa taifa naye wa nne akauawa barabarani mashariki mwa Paris.
'Ombeeni Paris' linasema bango hili lililoinuliwa na mwanafunzi kabla ya mechi kati ya Notre Dame Fighting Irish na St Francis Red Flash uwanja wa Purcell Pavillion mjini South Bend, Marekani. Hii ni baada ya mashambulio kuua watu zaidi ya 120.
Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa watu 200 wamejeruhiwa kwenye mashambulio yaliyotekelezwa Paris, 80 wamejeruhiwa vibaya
Gazeti la Le Parisien limeandika 'Cette fois, c'est la guerre' maana yake 'Wakati huu, ni vita'.
Limechapisha takwimu za waathiriwa wa mashambulio Ufaransa, ambazo linasema limepata kutoka kwa maafisa wa polisi.
Takwimu hizo ni kama ifuatavyo:
- Bataclan: watu 100 wamefariki, saba wamo hali mahututi, wengine wanne wanauguza majeraha
- Rue Charonne: 19 wamefariki, 13 hali mahututi, 10 wana majeraha
- Rue Bichat: 14 wamefariki, 10 wamo hali mahututi, 10 wengine wamejeruhiwa
- Avenue de la Republique: Wanne wamefariki, 11 wamo hali mahututi, 10 wengine wamejeruhiwa
- Stade de France: Wanne wamefariki, 11 wamo hali mahututi, wengine 39 wamejeruhiwa
- Rue Beaumarchais: watatu wamo hali mahututi, wanne wengine wanauguza majeraha
Shirika la habari la Associated Press limewanukuu polisi Paris wakisema wanaamini washambuliaji wote wameuawa. Kwenye shambulio la Bataclan, ambako watu 100 wanahofiwa kufariki, washambuliaji wanne walifariki.
Magazeti duniani yalivyoripoti habari za mashambulio yaliyotokea Paris na kuua zaidi ya watu 120
Miji mingine duniani imeimarisha usalama baada ya mashambulio kutokea Paris. Hawa, ni maafisa wa polisi jijini New York
Mghahawa wa Cafe la Bonne Biere ni mojawapo ya maeneo yaliyoshambuliwa. Hivi ndivyo hali ilivyo kwa sasa
No comments
Post a Comment