Ndugu Watanzania, Kama mnavyofahamu kuwa ibara ya 132(4) na (5) na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria namba 13 ya mwaka 1995 inataka viongozi wote wa umma kujaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni. Tamko hilo huwasilishwa Sekretariat ya Maadili ya Viongozi kabla ya mwisho wa kila mwaka. Kama nifanyavyo siku zote, nawajulisha rasmi kwamba nimetimiza matakwa hayo ya katiba na sheria kuhusu Maadili ya Viongozi.
Inafahamika kuwa Chama Cha ACT Wazalendo, kwa mujibu wa Katiba yake na Azimio la Tabora, kimeelekeza kuwa Viongozi wake wote waweke wazi kwa Umma Tamko la Mali, Madeni na Maslahi. Kwa kufuata masharti ya Katiba ya Chama Cha ACT Wazalendo natangaza rasmi fomu zangu nilizowasilisha Leo Sekretariat ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Ni matumaini yangu kwamba itafikia wakati Daftari la Rasilimali na Madeni la Viongozi wa Umma litakuwa linawekwa wazi kwa Umma ili wananchi waweze kujua Mali, Madeni na Maslahi ya Viongozi wao na pale ambapo kiongozi ametoa habari zisizo sahihi au kuficha mwananchi aweze kutoa Taarifa kwenye Sekretariat na Baraza la Maadili liweze kufanya kazi yake ipsavyo.
Mfumo wa kuweka wazi Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma ni mfumo endelevu na muhimu kwenye vita vita dhidi ya ubadhirifu na ufisadi. Mataifa kadhaa duniani hutumia mfumo huu ( public disclosure of leaders’ assets and liabilities) kuwezesha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Nchini Uingereza na Kanada kwa mfano, daftari la matamko ya Rasilimali na Madeni ya Viongozi lipo wazi kwa kila mwananchi kuona na huuzwa kwenye duka la vitabu la Bunge.
Namsihi Sana Rais John Pombe Magufuli kusaidia kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria ya maadili ya Viongozi ili kurejesha na kuboresha Miiko ya Viongozi katika kuimarisha vita dhidi ya ufisadi nchini. Rais aliahidi kuweka wazi Mshahara wake alipokuwa anazungumza katika kipindi cha 360 cha Clouds TV. Ninamkumbusha afanye hivyo na pia aweke wazi Mali, Madeni na Maslahi yake ya Kibiashara ili awe mfano kwa Viongozi wengine Nchini.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kigoma Mjini
30/12/201
No comments
Post a Comment