TANZANIA
Wanaohusika katika msururu wa vikao vya mashauriano ya mgogoro wa Zanzibar ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dokta Ali Mohamed Shein, ambaye ndiye mwenyekiti huku wajumbe wakiwa ni makamu wa pili wa rais balozi Seif Ali Iddi, marais wastaafu Amani Abeid Karume, Jakaya Mrisho Kikwete, Ali Hassan Mwinyi, Dokta Salmin Amour Juma na makamu wa kwanza wa rais Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye ndiye mwakilishi kutoka upande wa CUF.
Zanzibar iliingia katika mgogoro wa kisiasa miezi miwili iliyopita baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi visiwani humo Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura.
bbcswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
SYRIA
Vikosi vya jeshi la Syria vikisaidiwa na mashambulizi makubwa ya anga vimesonga mbele kuelekea mji muhimu wa jimbo la kusini la Deraa leo baada ya kukamata kituo cha karibu cha jeshi.
Jeshi la Syria limesema limerejesha katika udhibiti wake kambi ya jeshi ya brigedi ya 82, moja kati ya vituo vikubwa kaskazini ya mji unaoshikiliwa na waasi wa Sheikh Maskin, ambapo kukamatwa kwake na waasi mapema mwaka huu kulitishia kuzuwia njia za kulipatia jeshi hilo mahitaji kwenda upande wa kusini.
Jeshi pia limesema katika taarifa kwamba limekamata eneo la milima ya Al Hesh, kaskazini magharibi ya Sheikh Maskin. Eneo hilo la milima linaangalia sehemu kubwa inayodhibitiwa na waasi la Deraa magharibi.
Kwa upande wake Marekani na washirika wake wameshambulia maeneo ya kundi la Dola la Kiislamu kwa mashambulio 31 ya anga jana katika operesheni yao ya hivi karibuni dhidi ya wanamgambo hao nchini Iraq na Syria.
dwswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
IRAN
Iran imesema leo imeingia katika siku za mwisho za kukamilisha jukumu lake chini ya makubaliano ya kimataifa kuizuwia nchi hiyo katika mpango wake wa kinyuklia baada ya kusafirisha madini ya urani yaliyorutubishwa kwa kiwango cha chini kwenda Urusi.
Shirika la nishati ya atomic la Iran limesema tani 11 za madini ya urani zimepelekwa Urusi jana , hatua ambayo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema ni muhimu chini ya makubaliano hayo ya Julai 14 kati ya Iran na mataifa makubwa sita.
Kwa kufanya hivyo Iran sasa kwa kiasi kikubwa itapunguza kiwango kikubwa cha madini hayo ya urani, ambayo yalirutubishwa kwa kiwango cha juu, na ambayo yangeweza kutumika katika utengenezaji wa silaha za kinyuklia, lengo ambalo jamhuri hiyo ya Kiislamu inakana kutaka kufanya.
Kerry amesema hatua hiyo ya Iran kusafirisha madini hayo kwenda Urusi imesogeza mara tatu muda itakaoweza kuchukua kutayarisha madini hayo kwa ajili ya utengenezaji wa mabomu kutoka miezi miwili ama mitatu na kufikia miezi sita hadi tisa.
dwswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
UJERUMAN
Mahakama nchini Ujerumani, leo imemhukumu meya wa zamani wa Rwanda kifungo cha maisha gerezani, kutokana na mchango wake katika mauaji ya watu zaidi ya 400 mwaka 1994, wengi wao Watusti katika kanisa.
Mahakama ya juu ya kanda ya mjini Frankfurt, imesema Onesphore Rwabukombe mwenye umri wa miaka 58, Mhutu na meya wa zamani wa wilaya ya Mavumba, alikuwa miongoni mwa watu walioamrisha mashambulizi dhidi ya kanisa katika mji wa Kiziguro.
Rwabukombe alikutwa na hatia ya kusimamia mauaji hayo, kuita washambuliaji zaidi na kupanga utaratibu wa kuzisafirisha maiti na kuzitupa shimoni. Mahakama pia imeondoa uwezekano wa kumuachia mapema, ikisema alikuwa na mchango mkubwa katika kupanga mauaji hayo ya halaiki.
Kanuni ya sheria za kimataifa inabainisha kuwa mauaji ya kimbari yanaweza kuadhibiwa popote duniani, na siyo tu katika nchi yalikotendeka. Rwabukombe amekuwa akiishi Ujerumani tangu mwaka 2002 baada ya kutoroka Rwanda na kutafuta hifadhi Ulaya.
dwswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
UFARANSA
Mashambulizi ya Waislamu wenye itikadi kali dhidi ya jarida la masihara la Charlie Hebdo yameifanya Ufaransa kuwa nchi ya tatu hatari kwa waandishi habari mwaka 2015, ikiwa nyuma tu ya Syria na Iraq.
Hayo yamesemwa leo na shirika la waandishi wasio na mipaka RSF. Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Paris limesema katika taarifa yake ya mwaka kwamba waandishi habari 67 wameuwawa duniani kote mwaka huu.
Katibu mkuu wa shirika hilo la RSF Christophe Deloire ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wengi wao ni waandishi waliouwawa ili kuwazuwia kufanyakazi zao.
Waandishi habari wanane waliuwawa mjini Paris Januari 7 wakati Waislamu wenye itikadi kali wakiwa na bunduki waliposhambulia ofisi za jarida la Charlie Ebdo, shambulizi la kwanza la aina hiyo dhidi ya nchi ya magharibi.
Dwswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
GUINEA
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limeitangaza Guinea kuwa haina tena ugonjwa wa Ebola miaka miwili baada ya kuripuka, na kusambaza vifo katika mataifa ya Afrika magharibi na kuisukuma jamii ya eneo hilo iliyoathirika sana katika ukingo wa kuporomoka.
Taifa hilo ambalo ni moja kati ya mataifa masikini sana duniani, na koloni la zamani la Ufaransa lilipatikana na mgonjwa mmoja ambaye ni mtoto mchanga ambaye alikuwa mhanga wa kwanza wa ugonjwa huo, na maafisa wa afya waliweza baadaye kuorodhesha vifo 2,500.
Kiasi ya watu 11,300 walikufa kutoka idadi ya wagonjwa 29,000 walioorodheshwa, kwa mujibu wa shirika hilo la afya ulimwenguni ambapo wataalamu wengi wanaamini ni idadi ndogo kuliko athari halisi iliyosababishwa na ugonwa huo.
dwswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
AFGHANISTAN
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani ameahidi leo kuitisha uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa mwaka ujao, wakati akijaribu kutuliza mvutano wa kisiasa ambao unazuwia mapambano ya serikali yake dhidi ya wapiganaji wa Taliban.
Muda wa mwisho wa bunge ulipangwa kumalizika Juni 22 mwaka huu, lakini uchaguzi ambao ulikuwa ufanyike Aprili umeahirishwa kwasababu ya hofu ya usalama na kutokubaliana juu ya vipi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki baada ya uchaguzi wa rais ambao umebishaniwa vikali mwaka jana.
Iwapo uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa , utafanyika katika hali mbaya kabisa ya usalama, ambapo kundi la Taliban linatarajiwa kuendeleza kampeni yake ya mwaka huu ambayo ilihusisha kuukamata kwa muda mji wa Kunduz kaskazini mwa nchi hiyo.
dwswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
BURKINA FASSO
Takriban maafisa 20 wa kijeshi wamekamatwa nchini Burkina Faso baada ya serikali kutibua njama ya kumuachilia huru kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwezi Septemba.
Maafisa mjini Ouagadougou wanasema kuwa serikali ilitibua njama ya kumuachilia huru jenerali Gilbert Diendere.
Vyanzo vya afisi ya waziri mkuu Isaac Zida vinasema kuwa , maafisa hao walikuwa na nia ya kuwaachilia huru washukiwa wote wa mapinduzi mbali na kukirejesha kikosi hicho cha kumlinda rais kilichopigwa marufuku kufuatia jaribio hilo la mapinduzi.
Aliachia madaraka baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa umma na viongozi wa kikanda.
Kikosi chake kilichokuwa kikimlinda rais kimehusishwa na njama hiyo mbali na madai mengine mengi ya ukiukaji wa sheria na kwa ukatili uliotekelezwa wakati wa utawala wa rais Compaoré.
Njama hiyo imetibuka katika siku ambayo taifa hilo linamtarajia rais mpya kuchukua hatamu leo.
Rais huyo mpya Roch Marc Christian Kabore amesema kuwa ''sheria itafwata mkondo wake''
Waziri mkuu Zida amesema ''Tumewatia mbaroni ilikutoa ilani kuwa njama kama hiyo hainabudi ila kutibuka''
Jenerali Diendere na Compaore, wanakabiliwa na tuhuma za mauji ya rais wa zamani wa taifa hilo Thomas Sankara.
Wamekanusha madai dhidi yao.
Bbcswahili
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
No comments
Post a Comment