MKUU wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Farida Mgomi amepiga marufuku wakulima kuuza mazao yakiwa shambani.
Alisema hayo mjini hapa wakati alipofanya ziara ya kutembelea vijiji vya wilaya hiyo ambapo pamoja na mambo mengine alikagua hali ya mazao shambani.
Alisema sasa ni marufuku kwa wakulima kuuza mazao yakiwa shambani na kuwaagiza watendaji wa kata na vijiji kutenga maeneo kwa ajili ya kuyauza mazao hayo ili kukabiliana na hali ya njaa na pia halmashauri iweze kukusanya ushuru wa mazao.
"Ili kukabiliana na tatizo la njaa ni marufuku kwa wanunuzi wa mazao kuyanunua yakiwa mashambani na hakikisheni mnaweka vituo vya kuuza mazao ili halmashauri ipate ushuru" alisema
Alisema Wilaya hiyo imekuwa ya mwisho kitaifa katika ukusanyaji wa mapato na kwa kupitia njia hiyo itakuwa ni mmoja ya vyanzo vya mapato ya halmashauri.
Pia aliwataka wakulima kuhakikisha wanahifadhi chakula cha kutosha ili kuweza kuondokana na aibu ya kuwa ombaomba wa chakula kila mwaka.
"Tumekuwa tukiambiwa tunakula viwavi, zambarau na matunda ya porini jambo ambalo ni la aibu sana ukizingatia wilaya hii ndipo ilipo ikulu ya Rais" alisema
Pia alipiga marufuku upikaji pombe kwa kutumia mazao na kufanya sherehe ambazo zinatumia chakula kingi na wakati mwingine hazina manufaa yoyoye.
Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakifanya sherehe wakati wa mavuno huku nafaka nyingi zikitumika kupikia pombe na watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua.
Akizungumza katika tarafa ya Makang'wa alisema mwaka huu wamejiwekea mikakati kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda katika wilaya hiyo.
"Mwaka huu wa 2016 hatutaki kuona wanafunzi wakifeli katika wilaya hiyo, maafisa elimu, wakuu wa shule wajipange kuhakikisha watoto wanafaulu vizuri na kama wanashindwa basi waachie ngazi kwani hiyo ni fedheha" alisema
mwisho
No comments
Post a Comment