Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Machi 16, 2016) alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Chato waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wilayani Chato, mkoani Geita.
Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili akitokea mkoani Kagera, alisimamishwa na wakazi wa kijiji cha Kalebezo, kata ya Nyamirembe, wilayani Chato na kukuta mabango yaliyokuwa yakidai maji safi na kuelezea uharibifu wa pampu ya maji.
Katika maelezo yao, wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa maji kwenye kata hiyo ulishakamilika lakini pampu yao imechukuliwa na kupelekwa Morogoro jambo lililosababisha wakose maji kwa muda mrefu.
Kwa sababu alikuwa hajafika Chato mjini na hakuwa na taarifa sahihi za mradi huo wa maji, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba analibeba jambo hilo na atafuatilia hadi aelezwe ni kwa nini pampu hiyo imepelekwa Morogoro.
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ndipo suala la maji likaibuka tena na Waziri Mkuu kuamua kuchukua hatua hiyo.
“It’s unethical (ni kinyume cha maadili) kumdanganya kiongozi wako. Nimekuuliza mara mbili mbili kama una uhakika kuwa pampu hiyo ipo ukasema una uhakika kuwa ipo. Nimemtuma diwani na vijana wangu wakacheki wakasema hakuna pampu,” alisema Waziri Mkuu na kumwita Diwani huyo jukwaani ili atoe majibu.
“Pale kulikuwa na pampu mbili; moja ni ya kuvuta maji kutoka kwenye kina kirefu na kuyapeleka kwenye pump house na nyingine ni ya kuvuta maji kutoka kwenye pump house na kuyapeleka kwenye tenki kubwa la kuhifadhia maji. Ile ya kutoa maji kwenye kina kirefu ndiyo haipo, wataalamu wanajua wameipeleka wapi,” alisema Bw. Charles Manoni ambaye ni diwani wa kata ya Nyamirembe ambayo kijiji cha Kalebezo kimo.
Waziri Mkuu alisema ahadi ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu. “Lazima watumishi wa umma wabadilike na kuanza kuwatumikia wananchi kwa dhati. Hatuwezi kuwa na watumishi waongo ambao wanamdanganya hata Waziri Mkuu.”
“Kuanzia sasa, Engineer atakaa pembeni, polisi na TAKUKURU wamchunguze. Asitoke Chato hadi uchunguzi ukamilike. Nataka kujua nani alichukua hiyo pampu na kwa kibali gani. Tukijiridhisha atarudi lakini kwa sasa hivi akae kando,” alisema.
Mapema jana mchana, akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Geita na wilaya ya Chato mara baada ya kupokea taarifa zao kwenye ukumbi wa Halmashauri, Waziri Mkuu alimpa fursa Mhandisi huyo aeleze nini kimetokea kuhusu pampu inayodaiwa kupelekwa Morogoro lakini akakanusha na kudai kuwa ipo palepale kijijini.
“Una uhakika na hayo unayoyasema? Hiyo pampu ipo kweli kijijini? Nikienda nitaiona?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa mara mbili na mhandisi huyo kwamba ana uhakika asilimia 100 kwamba pampu ipo na wala haijaenda Morogoro.
Alipotaka kujua ni kwa wananchi wa kijiji kile hawana maji kutokana na ubovu wa pampu hiyo, alijibiwa kwamba mradi ule ulikuwa chini ya mamlaka ya maji ya mji wa Bukoba (MBUWASA) ambako wilaya hiyo ilikuwepo zamani kabla ya kuhamishiwa kwenye mkoa mpya wa Geita mwaka 2012.
Mhandishi huyo alisema amekuwa akifuatilia fedha za matengenezo kutoka kwa Mkurugenzi wa MBUWASA bila mafanikio, ndipo Waziri Mkuu akamuagiza aende nje ya ukumbi huo akapige simu na kumletea majibu ni lini fedha hizo zitapatikana ili wananchi wa kijiji kile waendelee kupata maji.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, MACHI 17, 2016.
No comments
Post a Comment