Mfano wa aina ya vyoo vinavyoweza kuonekana katika maeneo ya wilaya ya chamwino mkoani dodoma |
Na Peter Mkwavila,Chamwino.
WILAYA ya Chamwino imekosa maendeleo miaka kumi toka iundwe kutokana na wakuu wa idara, watendaji wa kata na vijiji kutumia muda mwingi kujiingiza kwenye migogoro mbalimbali,Mkuu wa wilaya hiyo Farida Mgomi alieleza jana
Akizungumza na watendaji na wakuu wa idara mbalimbali wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye wilaya hiyo ,alisema kwa kiasi kikubwa hali hiyo imesababishwa na uzembe wa viongozi na katika ngazi mbalimbali.
Aliongeza kuwa hata watendaji wa vijiji na kata imefikia hatua ya wanashindwa kuitisha mikutano ya kuwasomea mapato na matumizi kwa fedha wanazochangia wananchi juu ya masuala ya maendeleo.
“Inasikitisha sana pamoja na wilaya hii kuwa na miaka kumi toka iundwe lakini bado haina maendeleo,hii inasababishwa na nyinyi mliopewa dhamana kuchukua muda mwingi kujihusisha zaidi na migogoro badala ya maendeleo yanayohitajika kwa wananchi na kwa taifa”alisema..
Alisema vikao vya kushughulikia migogoro imekuwa vingi tofauti na vile vya kuleta maendeleo kutokana na asilimia kubwa ya viongozi waliopewa dhamana kuacha kujihusisha na masuala ya kimaendeleo kama vile ya ujenzi wa vituo vya afya,maabara,barabara na majengo ya madarasa huku ambavyo yamedorora.
Mkuu huyo alisema migogoro hiyo inapoteza muda na kamwe haiwezi kuijenga wilaya, hivyo watendaji ni muhimu wakawajibika katika kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili waondokane na mawazo hayo ambayo yamekuwa yakidhohofisha maendeleo.
Hata hivyo viongozi hao wa idara na watendaji wa vijiji na kata pia wameonywa kutotumia muda wao kwa kunywa pombe nyakati za kazi kwa kuwa hali hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha maendeleo kwa wananchi.
Alisema baadhi ya viongozi wakiwemo wakuu wa idara,kata hadi vijiji,wamekuwa wakihusisha kwa kutumia muda mwingi katika unywaji wa pombe bila kujali kuwa muda huo wanatakiwa kuwepo kazini.
Mwisho.
No comments
Post a Comment