Rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Giovanni
Infantino ameungana na mamilioni ya waombolezaji nchini Uganda kwa kutuma salamu
za rambi rambi kwa familia iliyompoteza kipa Abel Dhaira.
Ujumbe wa wa Infantino ulitumwa moja kwa moja kwa rais wa shirikisho la kandanda nchini Uganda FUFA bwana Moses Magogo wakati wa kusanyiko la ibada ya mazishi zilizofanyika mapema hii leo katika kanisa la All Saints Cathedral lililopo Nakasero jijini Kampala .
Aidha FUFA imesema kuwa limekuwa sio jambo la kawaida kupokea salam za rambi rambi kutoka FIFA kutoka haswa ikizingatiwa kuwa kumekuwa na vifo vya wachezaji wengi nchini humo.
Kipa huyo alifariki dunia Jumapili ya pasaka nchini Iceland kutokana na maradhi ya saratani ya tumbo.
Naye Rais wa Shirikisho la Kandanda barani Afrika CAF Issa Hayattou alituma salamu zake wiki iliyopita ambapo pia aliridhia ombi la FUFA la kutaka kuwepo kwa dakika moja ya ukimya kabla ya kupigwa kwa mechi ya kufuzu michuano ya AFCON kati ya UGANDA na BURKINA FASO.
Wengine waliohudhuria msiba huo siku ya leo ni pamoja na waziri wa michezo nchini Uganda, , Charles Bakabulindi, kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Milutin Sredojevic “Micho”, wachezaji wote wa timu ya taifa ya Uganda, Meya wa jiji la Kampala Elias Lukwago, wanafamilia ndugu jamaa na marafiki.
Jeneza lenye mwili wa Abel Dhaira litapelekwa kwenye uwanja wa mpira wa Nakivubo kwa heshima za mwisho ambapo baadaye atasafirishwa kuelekea Jinja kwenye nyumba ya baba yake kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Jumatano ya wiki hii.
No comments
Post a Comment