Kibaka akiwa amejinyonga kwenye nyumba ya mpangaji kata ya Malunga wilayani Kahama |
Mwili wa marehemu ukiondolewa eneo la tukio |
Kijana ambaye hajafahamika jina lake mara moja na anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 22-25 amefariki dunia kwa kujinyonga na shuka katika nyumba ya Therezia Francis mkazi wa Kata ya Malunga wilayani Kahama mkoani Shinyanga,baada ya kuvunja kufuli katika mlango wa chumba cha mpangaji aliyefahamika kwa jina la Frank na kuingia kwa lengo la kwenda kupora.
Afisa mtendaji wa Kata ya Malunga Cosmas Bukango ameiambia Malunde1 blog kuwa tukio hilo limetokea leo April 1,2016 majira ya saa 9.45 alasiri wakati mvua za masika zikiendelea kunyesha na watu wakiwa ndani.
Amesema wakati mvua inaendelea kunyesha mtu huyo anayedhaniwa kuwa ni kibaka alifika katika nyumba hiyo na kipande cha nondo kilichotumika kuvunja kufuli la mlango.
Bukango amesema kibaka huyo alifanikisha zoezi zima la kuvunja mlango huo, akaingia ndani ya chumba cha mpangaji ambaye alikuwa katika mihangaiko ya kutafuta mkate wa kila ukizingatia sasa ni kazi tu, ndipo jirani yake aliyefahamika kwa jina la Getruda Ziota aliyeshuhudia zoezi zima akaamua kufunga chumba kwa nje na kutoa taarifa kwa jirani zake anaoishi nao.
Hata hivyo Bukango ameuambia mtandao huu kuwa baada ya kupata taarifa hizo alifika katika eneo la tukio na kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi Mjini Kahama.
Wakati wanasubiri Polisi wafike hapo,kibaka huyo alichukua uamuzi wa kuchukua shuka na kupanda kitandani na kufunga juu ya dari na kujinyonga.
Polisi walipofika eneo la tukio walikuta kibaka amejinyonga na wakaondoka na mwili wa kibaka huyo.
Akisimulia tukio hilo, Getruda Ziota ambaye ndiye shuhuda ameueleza mtandao huu kwamba alikuwa ndani ya chumba chake akishona nguo na cherehani na kumuona mtu huyo akirandaranda katika mazingira na kuhisi ana lengo la kujikinga na mvua.
“Mvua ilipoanza kunyesha nilikaa ndani na kuanza kushona nguo,mara nikamuona mtu mmoja anakuja, akaingia maeneo ya chooni na akawa anachungullia kila sehemu,nikajua mtu huyu anajikinga mvua , kidogo nimuite aje ndani tukae naye ili asinyeshewe na mvua lakini roho ikasita, baada ya hapo nilimuona akizidi kusogea kwenye chumba cha jirani yangu.
“Baada ya hapo ikabidi nisimame juu ya sturi kwa kuwa pazia langu linaonyesha vizuri,nikamuona ametoa nondo akabenjua kufuri na mlango ukafunguka aliangaza sana na kuingia ndani ndipo nikamfungia kwa nje nikatoa na taarifa kwa jirani yangu nikamwambia jirani yetu ameingiliwa, pia niakaendelea kusambaza taarifa na baada ya watu kujaa tukashauriana tufungue mlango tumtoe nje kuingia ndani tukakuta mtu tayari amejinyonga na shuka,”amesema Ziota.
Jeshi la Polisi Kahama limethibitisha kuwepo kwa tukio hilo tukio hilo.
No comments
Post a Comment