Nyota ya muogeleaji wa kike wa Tanzania, Sonia Tumiotto imezidi kung’aa katika mshindano ya kutafuta tiketi ya kufuzu michuano ya Olimpiki baada ya kutwaa medali ya shaba mjini Dubai.
Katika mashindano hayo yajulikanyo kwa jina la ‘Dubai International Aquatics Championships’ Sonia alishinda medali ya shaba ambayo ni ya tatu kushinda kwa waogeaji wenye umri kati ya miaka 14 na 15.
Medali ya kwanza ya Sonia ilikuwa ya shaba ya mita 400 freestyle na baadaye kushinda ya dhahabu katika staili ya backstroke ya mita 50 na juzi alishinda medali ya shaba kwenye mita 200 freestule kwa kutumia muda wa 2.15.59.
Pamoja na kufanya vyema katika mashindano hayo, Sonia ambaye anatokea klabu ya Dar Swim Club (DSC) chini ya katibu mkuu, Inviolata Itatiro, bado hajapata tiketi ya kushiriki katika mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika jijini Rio de Janeiro mwezi wa Agosti.
Kwa mujibu wa muda wa kufuzu uliotolewa na shirikisho la kmchezo wa kuogelea la Dunia (Fina), Sonia alitakiwa angalau ashinde kwa kupata muda wa 2.03.13.
Sonia pia alimaliza katika nafasi ya nne katika mashindano ya katika mashindano ya mita 50 ya freestyle kwa kupata muda wa 30.46.
Mbali ya Sonia, muogeleaji wa kiume, Hilal Hemed Hilal naye alianza kung’ara katika mashindano hayo baada ya kumaliza katika nafasi ya nne katika mita 50 katika staili ya freestyle.
Pamoja na matokeo hayo, Hilal ambaye anatokea klabu ya Taliss, hakuweza kupata muda wa kufuzu katika mashindano ya Olimpiki.
Mbali ya Sonia na Hilal, waogeaji wengine wa timu ya Taifa ambao wapo Dubai kusaka tiketi ya kufuzu Olimpiki ni Collins Saliboko na Aliasghar Karimjee.
Katibu Mkuu wa klabu ya Dar Swim Club (DSC), Invioata Itatiro alisema kuwa waogeaji hao wamethubutu kuiweka nchi katika ramani ya kimataifa pamoja na changamoto nyingi za mchezo huo.
Inviolata alisema kuwa bado anaamini kuwa Tanzania itapata nafasi angalau moja ya kufuzu katika mashindano ya Olimipiki.
No comments
Post a Comment