Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imesikitishwa na kulani viakli matukio ya mauaji ya wazee kumi (10) yaliyotokea wilaya ya Nzega, mkoani Tabora kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2016.
Inaelezwa kuwa, miongoni mwa chanzo cha mauaji ya wazee ni imani za kishirikina, uchu wa kumiliki mashamba na visasi mambo ambayo Serikali imekuwa ikiyakemea vikali. Wizara inawataka wananchi kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Nzega, kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa mauaji haya wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali ili kuwa fundisho kwa watu wengine.
Wizara inasisitiza kwamba wazee ni binadamu, na wanayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Vitendo vya mauaji ya kikatili wanavyofanyiwa wazee vinasababisha hofu kubwa kwa wananchi. Mauaji hayo yanawakosesha amani na vinadhohofisha ari ya kufanya shughuli za za maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
Familia inayoishi na mzee anayewindwa, itatumia muda mwingi kutekeleza jukumu la ulinzi na hivyo kupunuza tija na uzalishaji wa mwananchi mmoja na familia kawa ujumla. Kwa kutambua hili Wizara inahimiza wadau wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika ulinzi wa wazee na kuboresha huduma zao ili kuelekeza nguvukazi katika uzalishaji.
Wizara inapenda kutoa pole kwa familia ambazo zimeguswa na mauaji ya wazee waliopoteza maisha kwa kuuawa kinyama.
Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wazee wana haki ya kuthaminiwa utu wao, kupata huduma stahiki, na kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza kuhatarisha maisha yao ikiwemo haki yao ya kuishi.
Aidha, Jamii ihakikishe kuwa wazee na wananchi wote, wanaishi katika hali ya usalama, amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Taifa letu.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 15/4/2016
No comments
Post a Comment