Rais John Magufuli ameshusha kodi ya mapato ya mshahara (paye) kwa wafanyakazi kutoka asilimia 11 mpaka asilimia tisa. Rais Magufuli alitangaza punguzo hilo leo mjini Dodoma alipokuwa akihutubia kwenye siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa imefanyika Dodoma.
Amesema wafanyakazi wamekuwa waaminifu katika kulipa kodi ambayo inachangia kwenye maendeleo ya taifa kupitia mishahara yao. Alisema kwa kuwa bado vita dhidi ya wafanyakazi hewa na ufisadi inaendelea, ataangalia namna ya kuboresha mishahara yao hapo baadaye.
“Niliwaahidi wakati wa kampeni zangu kuwa nitapunguza kodi ya mapato kwenye mishahara yenu; sasa natamka kuwa nashusha kodi kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa. Najua punguzo hilo litakuwa limeacha pengo kwa serikali, lakini tutaangalia vyanzo vingine vya mapato vya kujazia hapo,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu wafanyakazi hewa, Rais amesema mpaka jana idadi ya wafanyakazi hewa imefikia 10,295. Amesema wafanyakazi hao hewa wamelipwa zaidi ya Sh 11 bilioni na kama wangeendelea kuachwa kwa mwaka mzima wangelipwa zaidi ya Sh 139 bilioni. Rais Magufuli ameapa kuwashughulika popote walipo.
Pia amewaagiza waajiri wote nchini kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wao na kuhakikisha wanapeleka michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii bila kukosa.
sikiliza alichokisema hapa>>>
No comments
Post a Comment