WASANII WA ORIJINO KOMEDY WAKAMATWA NA POLISI
Wasanii wanne wa kundi la vichekesho la Orijino Komedi akiwamo meneja wao wamekamatwa na kuhojiwa na jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kosa la kuwa na sare za polisi.
Juzi, jeshi hilo lilitoa onyo kwa mtu ama kikundi chochote kuacha kutumia mavazi yanayofanana na sare zinazovaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama nchini na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
SERIKALI KUCHUNGUZA
MALI ZA VIGOGO 500
WAKATI takribani asilimia 20 ya viongozi wa umma kwa mwaka 2011 hadi mwaka jana hawakuwasilisha matamko ya mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa wakati, mwaka huu serikali imetangaza kuhakiki matamko ya mali za viongozi 500.
Aidha, serikali hiyo imebainisha wazi kuwa haitowafumbia macho viongozi, watakaoshindwa kuwasilisha matamko ya mali zao kwa mujibu wa sheria, ikiwemo viongozi watakaowasilisha matamko ya mali yatakayobainika kuwa na udanganyifu.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki wakati akifungua warsha ya wadau, kujadili taarifa ya matokeo ya utafiti kuhusu hali ya maadili nchini Dar es Salaam jana.
TUNDU LISSU ATUMIA
DAKIKA 120 KUPANGUA HOJA MAHAKAMANI ........
Tundu Lissu, ambaye ni wakili wa Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya jana alitumia muda wa saa mbili kupangua maombi ya wananchi wanne wanaopinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi mteja wake.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa tena baada ya Mahakama ya Rufaa kufuta uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali hoja za kupinga matokeo hayo, ambazo ziliwasilishwa na wafuasi wanne wa aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, Steven Wasira (CCM).
Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu, alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubali pingamizi la Lissu kuwa wafuasi hao hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi hiyo.
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na maofisa wengine saba waandamizi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 27 yakiwamo ya matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Washitakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara, Avelin Momburi, Meneja wa Fedha na Uhasibu, Benamini Mwakatumbula, Meneja wa Bajeti na Milki, Joseph Makani, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Wengine ni Xavery Kayombo ambaye wadhifa wake haukutajwa, na Astery Ndefe ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers Company Limited. Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka yanayohusu kutumia nyaraka zenye kusudio la kudanganya na kula njama za kutenda kosa.
ZAIDI YA WATU 40,000 WANASHIKILIWA UTURUKI
Waziri Mkuu wa Uturuki, amesema zaidi ya watu 40,000 wanashikiliwa na Polisi wakihusishwa na jaribio la kuipindua Serikali ya nchi hiyo.
Katika hotuba yake ya moja kwa moja katika Televisheni, Binali Yildirim pia alisema takriban wafanyakazi wa sekta ya Umma 80,000 wamefutwa kazi wakiwemo wanajeshi,Polisi na watumishi wa Umma.
No comments
Post a Comment