Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) EX Peter Kakamba amefariki dunia alfajiri ya tarehe 30/11/2016 katika hospital ya taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kakamba alizaliwa mwaka 1963 katika kijiji cha Kawajense Wilayani Mpanda, mkoa wa Katavi. Alisoma shule ya msingi Shanwe Kawajense mwaka 1973 hadi 1980, Kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule ya Sekondari Kantalamba mwaka 1981 hadi 1984 ambapo kidato cha tano na sita alisoma katika shule ya Sekondari Umbwe mkoani Kilimanjaro mwaka 1985 hadi 1987. Mwaka 1992 hadi 1994 alisoma Astashahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 1988 ambapo katika utumishi wake alipandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo Konstable wa Polisi (1989), Sagenti wa Polisi (1991), Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1997), Mkaguzi wa Polisi (2003), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (2006), Mrakibu wa Polisi (2008), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (2011), Kamishna Msaidizi wa Polisi (2015) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2016).
Baadhi ya nafasi alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Mwendesha Mashtaka wa Polisi katika mkoa wa Iringa, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi, Afisa mnadhimu wa Polisi katika Mikoa ya Iringa na Geita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa na mpaka anafariki alikuwa Kamanda wa Polisi katika mkoa wa Singida.
Kufuatia kifo hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu anatoa pole kwa Maofisa, Wakaguzi,Askari, ndugu, jamaa na marafiki kwa Msiba huo.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa,
Jina la Bwana lihimidiwe - Amen.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba - ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments
Post a Comment