Serikali imesema ipo katika hatua za
mwisho za kuanza ujenzi wa Barabara ya Loliondo- Mto wa Mbu yenye urefu
wa KM 218 itakayojegwa kwa kiwango cha lami ili kurahishisha usafiri na
usafirishaji wa mizigo kwa wananchi wa mikoa ya Mara, Manyara, Arusha
na Mwanza.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika kijiji cha Sale,
wilayani Ngorongoro mara baada ya kukagua barabara hiyo ambayo ni kiungo
kati ya mikoa hiyo minne na nchi jirani ya Kenya.
“Tumeshatangaza Zabuni kwa ajili ya ujenzi
wa barabara hii, mapema mwakani zitafunguliwa ili kumpata mkandarasi
ambae atajenga barabara hii kwa kiwango kilichobora”, amesema Waziri
Prof. Mbarawa.
Aidha,Waziri huyo amefafanua kuwa ujenzi
wa barabara hiyo utatekelezwa kwa awamu mbalimbali ambapo awamu ya
kwanza itahusisha ujenzi wa barabara ya kutoka katika kijiji cha Waso –
Sale yenye urefu wa KM 49.
Ameongeza kuwa barabara hiyo ikikamilika
itaungana na ile ya Makutano-Nata yenye urefu wa KM 50 iliyopo Wilaya ya
Butiama, mkoani Mara na itasaidia kupunguza kero ya usafiri na kufungua
mikoa hiyo kibiashara kwa wakazi wa maeneo hayo.
Amewataka wananchi wa maeneo hayo kutoa
ushirikiano kwa mkandarasi atakayepata zabuni hiyo ili kumrahisishia
kumaliza mradi huo kwa wakati na viwango vinavyokubalika.
Kwa upande wao wakazi wa Kijiji cha Sale
wamemuelezea Waziri Changamoto wanazozipata katika barabara hiyo na
kuiomba Serikali kuharakisha mradi huo kwani utasaidia kuongeza pato
katika Sekta ya Utalii na kurahisisha huduma za kijamii.
“Barabara hii ni ya muhimu sana kwani
tumeteseka kwa muda mrefu, huduma za kijamii kama kumsafirisha kutoka
nyumbani mpaka kwenye kituo cha afya ilikuwa ikituchukua muda mrefu
kutokna na ubovu wa miundombinu”, amesema Bw. Elias Badiani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments
Post a Comment