WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba ameitaka Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kusitisha kila wanachokifanya katika eneo la mnada wa Pugu.
Kwa sasa manispaa hiyo inapima na kugawa viwanja. Alisema kitendo wanachofanya cha kugawa viwanja vya makazi kwa wananchi kunasababisha utapeli na uvamizi kwa eneo hilo.
Aliwataka wananchi waliotapeliwa kwa kupewa viwanja katika eneo hilo waondoke na kama ikibidi wawatafute waliowatapeli waweze kuwalipa. Nyumba zaidi ya 30 ni za kudumu na zipo za muda.
Dk Tizeba alisema hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea mnadani hapo na kubaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuvamiwa kwa kiwango kikubwa kwa eneo la mnada huo huku wafugaji wanaoleta mifugo yao kwa ajili ya kuuza wakikosa malisho.
Kuhusu kuvamiwa alisema ameelezwa na uongozi wa eneo la mnada huo kuwa Manispaa ya Ilala ni moja ya taasisi iliyohusika kuuza na kupima viwanja kwa ajili ya kuwapa wananchi, huku akihoji uhalali wa aliyeweza kupima ramani juu ya ramani katika eneo hilo.
“Waliopima eneo hilo ni mapateli, watafutwe haiwezekani kukawa na hali hiyo, hata huyo aliyechora ramani juu ya ramani huku akikuta kuna alama za mipaka na akaendelea kufanya hivyo atafutwe,” alisema Dk Tizeba na kuongeza kuwa hatua hiyo ni kuchonganisha wananchi na Serikali yao.
Kuhusu masharti ya mnada, alisema upo upungufu katika kuzingatia masharti ya mnada huo na kwamba ipo haja ya kuzungumza na mamlaka ya nyama nchini ili iweze kuona uwezekano wa kutoa bei elekezi ya nyama ili kila jambo liweze kufanyika kwa haki kila mmoja akinufaika.
Pamoja na maagizo hayo pia ameutaka uongozi wa mnada huo kuanza kutumia mzani kwa ajili ya kupimia nyama ili wanunuzi na wauzaji waweze kunufaika.
Dk Tizeba aliwataka wafanyabiashara wa ng’ombe kutopeleka ndama katika mnada huo kama wanavyofanya kwa sasa kwa sababu kufanya hivyo ni kuwalazimisha walaji kutumia mifugo ambayo haijafikia muda wake.
Aliwaelekeza kupeleka ndama katika minada ya awali ambako ndiko wafugaji wanaweza kupatikana na sio katika mnada huo kwa kuwa huo ni kwa ajili ya kuchinja peke yake.
Kuhusu kutumia mzani wa kupimia nyama, alisema alielezwa kuwa wafanyabiashara wa nyama ndio ambao hukataa kutumia, lakini watambue kuwa jambo hilo linaweza kuwasababishia hasara kuwa kuwa wanapima uzito wa ngombe kwa macho.
Awali kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Abdallah Temba alisema uvamizi katika eneo hilo ni kwa asilimia 99 na kwamba wanaziomba mamlaka zinazohusika kuwaondoa wavamizi katika eneo hilo ili liweze kutumika kama ilivyokusudiwa tangu awali.
Hata hivyo alisema kwa siku huingia ng’ombe zaidi ya 6500 katika mnada huo, huku kila moja ikilipiwa ushuru wa sh 5000 ambapo mapato yamekuwa yakiongezeka katika mnada huo.
No comments
Post a Comment