Serikali ya Kuwait imeahidi
kuipatia Tanzania mkopo wenye riba nafuu wa dola za Kimarekani Milioni
34 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 85 kwa
kiwango cha lami kutoka eneo la Chaya hadi Nyahua mkoani Tabora.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es
salaam na mwakilishi wa Balozi wa Kuwait hapa nchini, Bw. Mohammad
Rashid Alamiri, aliyeongoza ujumbe kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait,
ulipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi na
kijamii kati ya Tanzania na Kuwait.
Dkt. Mpango ameushukuru Mfuko wa
Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund) kwa kuipatia Tanzania mkopo wenye
masharti nafuu utakaochochea maendeleo kwa Watanzania hususani wanaoishi
maeneo hayo kutokana na umuhimu wa barabara katika kukuza uchumi wa
Taifa.
Amesema kuwa kipande hicho cha
barabara kutoka Chaya hadi Nyahua, ambacho kiko Barabara Kuu itokayo Dar
es salaam kwenda katika mikoa ya Tabora na Kigoma, licha ya umuhimu
wake katika kukuza biashara na usafiri na usafirishaji wa abiria na
mizigo ikiwemo inayokwenda nchi jirani, ilikuwa haijapata fedha kwa
ajili ya ujenzi wake.
“Riba waliyoiweka mezani kwa
mazungumzo ni asilimia 2 lakini nimewaomba waangalie uwezekano wa
kuiteremsha walau ifikie asilimia 1.5 na wamependekeza kipindi cha
kuanza kulipa mkopo kiwe miaka ishirini ijayo lakini nimewaomba wasogeze
hadi kufikia miaka 25 kama ilivyo kwa mradi wa Hospitali ya Mnazimmoja”
aliongeza Dkt. Mpango
Dkt. Mpango amesema Serikali ya
Kuwait kupitia Mfuko wake huo wa Maendeleo wameonesha nia ya kutoa mkopo
wenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya
Mnazi Mmoja iliyoko Visiwani Zanzibar.
“Nawahakikishia kuwa baada ya
muda si mrefu wananchi wa mikoa ya Tabora na Kigoma watarajie kuona
mkandarasi akiingia kazini ili kujenga barabara hii muhimu sana kwao na
kwa uchumi wa Taifa kwa ujumla” Alisisitiza Dkt. Mpango.
Ameeleza kuwa ujenzi wa kipande
cha barabara hiyo kutoka Chaya hadi Nyahua unatarajia kugharimu
shilingi Bilioni 61 lakini Kuwait haitatoa fedha zote hivyo ameuomba
Mfuko huo uangalie uwezekano wa kutoa kiasi hicho chote cha fedha ili
uweze kukamilika mapema.
No comments
Post a Comment