TANZANIA ina gesi asilia ya kujitosheleza na ya ziada, hivyo inaangalia namna ya kuiuza gesi hiyo kwenye soko la dunia.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura), Felix Ngamlagosi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa sekta ya gesi, ulioandaliwa na mamlaka hiyo.
“Hatuwezi kuingiza nchini gesi wakati tunayo nyingi, kinachofanyika sasa ni kuangalia namna ya kuisafirisha gesi yetu kwenda kwenye soko la dunia na Wizara pamoja na serikali inafanya kazi hiyo,” alisema Ngamlagosi.
Ngamlagosi alisema mazungumzo yanaendelea kati ya Serikali na wadau mbalimbali, kutafuta namna nzuri na wapi pa kuwekeza katika viwanda vya kusindika gesi na kupeleka katika masoko ya dunia.
Mkutano huo ulioandaliwa na EWURA, unawakutanisha wadau wa gesi ya asili, kujadili bei ya bidhaa hiyo kwaajili ya matumizi ya miradi ya kimkakati katika viwanda vitakavyotumia gesi kuendesha shughuli zao katika viwanda vya saruji na mbolea.
Oktoba 7 mwaka huu Wizara ya Nishati na Madini ilitangaza Kanuni mpya za upangaji wa bei ya gesi asili kwa matumizi mbalimbali. Ngamlagosi alisema mapendekezo ya EWURA ni kwenye viwanda vya saruji uniti moja ya gesi iuzwe kwa dola 4.25 na upande wa wazalishaji wa mbolea uniti moja ya gesi iuzwe dola 2.60.
“Kwanza tumewaeleza misingi tunayopaswa kuitumia kukokotoa bei hiyo ni ipi, wadau sasa wataleta maoni yao kwa maandishi ambayo tutayapokea na kuyafanyia kazi,” alisema Ngamlagosi.
Aidha, alisema baada ya kupokea maoni yao, yatajumuishwa katika maamuzi ya mwisho yatakayotolewa Desemba 31 mwaka huu, ambapo alisema awali Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) walikuwa wakikusanya maoni wao kutoka kwa mtu mmoja mmoja.
“Hiyo sasa ni mada chokozi tumeitoa, tunataka sasa TPDC watuletee maoni yao kama wanadhani bei hiyo ni sawa au si sawa, wauzaji wa saruji walete maoni yao, wauzaji wa mbolea walete na waeleze kwa vielelezo kwa nini inafaa na kwa nini haifai,” alisema na kuongeza kuwa maoni hayo yanakusanywa tangu Desemba 20 mpaka 27 mwaka huu.
Alisema kanuni zilizotolewa, zinaangalia pia umbali kutokea kwenye gesi inakotokea baada ya kuchakatwa na pia Serikali imeamua kutoa bei maalumu kwa miradi ya uzalishaji wa mbolea kwa sababu nchi inategemea kilimo.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipongeza kuwepo kwa mkutano huo ambao unapokea maoni ya wadau katika sekta hiyo.
“Tanzania sasa tunahamia katika nchi ya viwanda, miongoni mwa vitu muhimu ni nishati, na hiki kilichofanyika hapa ni kuangalia ni namna gani tunawashirikisha wadau wetu katika sekta hiyo katika kupokea maoni yao na kuyajumuisha katika maamuzi ya serikali ni jambo zuri,” alisema Mgandilwa.
No comments
Post a Comment