WAZIRI mwandamizi wa serikali ya Tanzania kwa awamu nne za uongozi, Stephen Masato Wassira, kupitia kwa wafuasi wake watatu, amekata rufaa Mahakama ya Rufaa, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kuhalalisha ushindi wa Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema).
Wassira (71 ) alikuwa waziri kwa mara ya kwanza tangu Desemba 07, 1973 akiwa naibu waziri wa Kilimo na ameendelea kuwa kiongozi mwandamizi wakati wa serikali ya Mwalimu Julius Nyerere, akarithiwa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, baadaye Rais Benjamin Mkapa na hatimaye uongozi wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete.
Tayari wafuasi hao wa Wassira; Magambo Masato, Matwiga Matwiga na Ascetic Malagaila, wamefungua kesi hiyo na imesajiliwa katika ofisi za mahakama ya rufaa jijini Mwanza tarehe 16 Desemba, 2016 na itakuwa ni kesi ya rufaa namba 199 ya mwaka 2016.
Katika rufaa hiyo iliyoandikwa na wakili wao, Constatine Mutalemwa, wametoa sababu kadhaa kama hoja zao za kukata rufaa.
Kwanza, wanadai kwamba jaji hakuzingatia makosa yaliyofanyika baada ya zoezi la kupiga kura.
Pili, Wassira au wakala wake wanadai hakuitwa kwenye majumuisho kujulishwa siku, mahali wanafanyia majumuisho.
Tatu, wanadai kuwa jaji hakutilia maanani kesi zinazofanana na hii zilizotolewa kama mfano mahakamani.
Nne, Jaji alikosea kutoa uamuzi kwa misingi ya maoni binafsi badala ya kuzingatia mambo ya maana.
Wanadai kuwa jaji alisema wananchi wa Bunda ni maskini waachwe wafanye shughuli za maendeleo kwa sasa.
Tano, wanadai jaji alikosea kuamua kuhusu sheria ya viapo na matamko iliyotajwa katika kanuni za kuendesha kesi za uchaguzi.
Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitoa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wassira (CCM).
Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, mkoani Mara.
Mahakama hiyo ilieleza kutoridhishwa na ushahidi wa kupinga matokeo hayo uliowasilishwa na upande wa walalamikaji, hivyo ikamthibitisha Bulaya kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.
Kesi ya kupinga matokeo hayo ilifunguliwa na wafuasi wa Wassira ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuondolewa kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji ambao ni wakazi wa Bunda walidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kwakuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanaemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.
Katika kesi hiyo, Bulaya alitetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
Credit: FikraPevu
No comments
Post a Comment