Mwenyekiti wa CUF anayetambulika na msajili wa Vyama vya Siasa Prof. Ibrahim Lipumba leo May 4, 2017 kupitia kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds TV amesema hakuwa na namba ya Edward Lowassa wakati anajiunga UKAWA.
Aidha, kwenye mahojiano hayo Prof. Lipumba amesema kuwa amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaiongoza CUF katika kudai haki za wananchi tofauti na Maalim Seif ambaye mara kadhaa ikitokea suala hilo haonekani akisema:
“Mwaka 2000 baada ya Uchaguzi Mkuu tuliingia kwenye maandamano Zanzibar, lakini Maalim Seif alikwenda Uingereza nilikuwa mstari wa mbele.
Prof. Lipumba amesema pia kuwa Maalim Seif amekuwa akidai kila anapokosana na mtu kisiasa kuwa mtu huyo anatumiwa na CCM akitolea mfano wa Ahmad Rashid, akisema:
“Ni kawaida ya Maalim Seif, akikosana na mtu kisiasa anasema anatumiwa na CCM. Rejea mgogoro na Ahmad Rashid".
Akizungumzia kuhusu kumpokea na kumtambulisha kwa viongozi wa UKAWA aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa wakati anatoka CCM, Prof. Lipumba alisema:
“Mbatia ndiye aliyeniunganisha na Lowassa. Sikuwa na namba zake, na wakati anakuja, nilisema wazi suala la rushwa ni mfumo siyo mtu.
“Mzigo mzito anapewa Mnyamwezi, lakini huu wa kumnadi Edward Lowassa ulinizidi uzito, nisingeweza kuubeba."
Wakai huo huo Prof. Lipumba amebainisha kuwa hakuwa na nia ya kurejea katika nafasi yake ya Uenyekiti wa CUF baada ya kujiuzulu, lakini aliombwa na wanachama wa chama hicho.
“Sikuwa na nia ya kurudi kuwa Mwenyekiti CUF ila wanachama waliniomba nirudi baada ya uchaguzi kumalizika na hali kutulia”
No comments
Post a Comment