Wakati diwani wa saba wa Chadema akijiuzulu jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema hata yeye kama angekuwa na moyo mwepesi na mpenda fedha, angekuwa ameshahama upinzani.
Mbowe alisema jana kwamba kuwa kiongozi wa upinzani awe mbunge, diwani, au mwenyekiti wa mtaa, kunahitaji roho ngumu na kwamba hiyo si kazi ya watu wenye kupenda fedha, bali ni ya maumivu, kudhalilishwa, kunyimwa ushirikiano, kufungwa wakati wowote na kunahitaji msimamo wa hali ya juu.
“Upinzani ni wito, wenye roho nyepesi hawawezi, kama ningekuwa napenda fedha, nina roho nyepesi, ningeshachukua hizo pesa na ningeshakimbia kabisa upinzani,” alisema.
Mbowe amesema hayo wakati chama hicho kikipitia misukosuko ya madiwani wake wa Mkoa wa Arusha kukihama na jana ilikuwa zamu ya Diwani wa Ambuleni, Arumeru, Japhet Jackson.
Diwani huyo aliwasilisha barua yake ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri jana mchana pia kama wenzake sita, akisema anamuunga mkono Rais John Magufuli.
Diwani wa karibuni kujiuzulu wa Ngobobo, Solomon Laizer pia wa wilaya hiyohiyo katika jimbo linaloongozwa na Joshua Nassari wa Chadema.
Akizungumza kwa simu jana, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema wanaowania nafasi za uongozi na viongozi wa Chadema wanahitaji kuwa na msimamo wa hali ya juu.
“Mara nyingi wanaowania nafasi kwa upande wa upinzani, ni wale waliokomaa, lakini katika uchaguzi uliopita, chama kilichopata watu wengi ni Chadema. Kutokana na mfumo huo wa kuwafungulia milango, wakaingia wengi, mbu, mende na mambo mengine,” alisema.
Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alidai kwamba kuondoka kwa madiwani hao wa Chadema kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa Serikali hasa wakuu wa wilaya ambao wanataka kumfurahisha Rais.
“Inashangaza kuona wote wanaojiuzulu wanatoa kauli moja ya kumsifu Magufuli, ina maana hawana sababu nyingine labda pengine Chadema kuna matatizo, sera zao mbovu, kuna hiki na hiki hakijakaa sawa,”alisema.
Aliongeza kuwa juhudi za kuwarubuni viongozi wa Chadema zipo katika majimbo yote ya Chadema na juhudi hizo zinapata nguvu zaidi mahali ambako kuna mkuu wa wilaya dhaifu ambaye anatumia nguvu za ziada.
Alisema wamebaini kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya ndiyo wanaotumiwa na wamewekwa kwa makusudi kwa ajili ya kuua upinzani nchini.
“DC anawahimiza wanachama na viongozi eti wapeleke barua za kujizulu kwake, kwa sababu ana jeuri ya mamlaka. Kisheria hana mamlaka ya kupokea barua ya kujiuzulu kwa mwanasiasa. Tumebaini hawa baadhi ya watendaji wanatumiwa na kuahidiwa makubwa endapo watawadhibiti wapinzani,” alisema.
Alisema walipata tetesi za kujiuzulu kwa madiwani hao lakini hawakutaka kuchukua uamuzi wa kuwafukuza kwani si vizuri kuishi kwa tetesi lakini kwa kuwa wameamua kuondoka anawatakia kila heri.
Alisema baadhi ya madiwani hao walionekana kwenye vikao vya CCM na kusema mtu anayezidiwa akili na kudanganywa kwa fedha hata akibaki katika chama hatakuwa na maana.
“Kuliko kubaki na watu wengi wanaopenda fedha, wanaohadaiwa kwa rushwa, bora tubaki watu wachache wenye maadili,” alisema.
Mbowe alisema, licha ya Serikali kuudhofisha upinzani, chama hicho kinaamini kuwa safari yake ni kama ya treni ya kwenda Kigoma ambayo wapo wanaopanda na wanaoshuka.
“Bado tunavuna maelfu ya wana CCM, alianza Edwin Mtei, lakini sasa tunazungumzia wanachama zaidi ya milioni sita. Muelewe kuwa upinzani haudhoofiki, bali unakua,” alisema.
Alisema wale waliodhani watapata ulaji kama wa fedha, ndiyo wanaokuwa wepesi kuondoka na kwenda kutafuta wanachokitaka.
“Tuna imani watabaki wachache wenye imani na nafasi za walioondoka zitachukuliwa na wengine walio bora zaidi,” alisema.
Kuhusu kuswekwa rumande kwa saa 48 kwa amri za wakuu wa wilaya, Mbowe alisema sheria za kumuweka ndani kiongozi zina masharti yake.
“Kuna utaratibu wa kufanya.DC sio polisi, anaweza kuagiza polisi, kamkamateni fulani kisha mumhoji na kisha afunguliwe mashtaka, lakini si kumuweka ndani kwa saa 48. Haya maagizo yote yanatolewa na ngazi za juu. Sisi sasa tunawashtaki hao Ma-DC wote na hata mimi nimemshtaki DC wa Hai, kwa kuharibu miradi yangu,” alisema.
No comments
Post a Comment