HABARI KAMILI
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imevitoa wasiwasi vyama vya siasa kuwa hakutakuwepo na wizi na
udanganyifu wa kura katika matokeo ya uchagauzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani unaotarajia kufanyika nchini tarehe 25 Oktoba, mwaka huu.
AIdha NEC imesema ipo tayari kushirikiana na wataalamu wa vyama
hivyo katika kubaini vyanzo vya wizi wa kura iwapo tatizo hilo
litajitokeza na hivyo kuhakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote
vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne (Septemba 29, 2015) Jijini Dar es
Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Damian Lubuva wakati wa mkutano
wake na wawakilishi wa vyama vya watu wenye ulemavu aliokutana nao kwa
ajili ya kupata ushauri na maoni ya taasisi hizo kuelekea uchaguzi mkuu
mwezi oktoba mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema hadi kufikia sasa, vyama vyote vyote
vinavyoshiriki uchaguzi huo vimefanyika kampeni za kistaarabu ingawa
katika siku za hivi karibuni baadhi ya vyama vimekuwa vikitoa kauli na
matamshi yaliyovuka mipaka, ambapo NEC imevionya vyama kuacha mara moja
tabia hiyo.
“Vipo baadhi ya vyama vya siasa na wagombea wao wamekuwa
wakitumia muda mwingi kutoa lugha zisizofaa baada ya kunadi sera ya
vyama vyao, vyama hivyo tumekutana nao na kuwataka kuacha mara moja
kampeni za aina hiyo” alisema Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva alisema tarehe 27 Julai mwaka huu, vyama vyote vya
siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu vilisaini maktaba wa maadili ya
uchaguzi huo, hivyo ni wajibu wa vyama hivyo kuzingatia viapo walivyotoa
katika maktaba huo.
Akifafanua zaidi Jaji Lubuva alisema iwapo chama chochote hakina
hoja ya kuzungumza na wananchi ni vyema kikawa kimya hadi siku ya
uchaguzi tarehe 25 Oktoba mwaka huu.
Aidha Jaji Lubuva alivitaka vyama vya siasa kuacha tabia ya
kuingilia masuala ya utawala ya tume hiyo, kwani kwa kufanya hivyo vyama
hivyo vitakuwa vikifanya kazi za tume hiyo na hivyo kuingilia masuala
ya ndani ya kiutendaji ya taasisi hiyo.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi huo, Jaji Lubuva alisema
mahitaji yote ya msingi ya uchaguzi huo tayari yamepokelewa na NEC ikiwa
karatasi, wino, na masanduku ya kura ambapo baadhi yake yameanza
kusafirishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kuhusu Daftari la kudumu la wapiga kura, Jaji Lubuva alisema
katika kipindi cha siku 10 zijazo kuanzia sasa Tume hiyo inatarajia
kusambaza daftari la kudumu katika mikoa yote nchini na wananchi
watatakiwa kuhakiki majina yao katika kipindi cha siku 8.
No comments
Post a Comment