Serikali ya Tanzania na Poland
zimeingia makubaliano ya ushirikiano yatakayosaidia kukuza sekta ya
kilimo kwa kuwawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo kupitia
Kampuni ya kutengeneza Matrekta ya Ursus kutoka nchini Poland
itakayoanza kufanya kazi zake nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka 2016.
Akizungumza mara baada ya
kufanyika kwa mkutano wa makubaliano hayo kati ya Serikali ya Tanzania
na ujumbe wa wataalam wa kilimo kutoka nchini Poland ulioongozwa na
Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi. Zofia Szalczyk jana
jijini Dar es salaam, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen
Wasira alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kuinua sekta ya kilimo na
kurahisisha upatikanaji wa matrekta hapa nchini.
Alisema Kampuni ya kutengeneza
Matrekta ya Ursus kutoka Poland imepewa jukumu la kuleta vipuri vya
matrekta na kuviunganisha hapa hapa nchini ikishirikiana na Shirika la
Uchumi na Maendeleo la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).
“Tumeingia mkataba na Seikali ya
Poland ili kuinua na kuimarisha sekta ya kilimo nchini kupitia
uundwaji wa matrekta haya hapa nchini, kazi hii itasaidia kupunguza
kilimo cha jembe la mkono ambacho kinafikia asilimia 62 na asilimia
38 iliyobaki inajumuisha kilimo cha jembe la kukokotwa na wanyamakazi
“plau” pamoja na matrekta” Alisema.
Aliongeza kuwa Serikali
itawajengea uwezo SUMA JKT ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo
na kuondoa hali iliyopo ya uagizaji wa matrekta yaliyounganishwa
ambayo hutumia gharama kubwa na kusababisha wakulima wengi hushindwa
kumudu gharama ya kuyanunua.
“Wakulima wataunganishwa na
Benki ya kilimo nchini kwa kupewa mikopo mbalimbali ya kununua vifaa vya
kutendea kazi mbegu pamoja na mbolea ili kukifanya kilimo kiwe cha
kisasa zaidi” alisema Wasira.
Wasira alisema kuwa Maghala
yaliyopo nchini yanauwezo wa kuhifadhi chakula tani 240,000 baada ya
kukamilika ujenzi wa maghala hayo kutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani
446,000 za chakula ambapo zitatumika Dola za Kimarekani milioni 110
katika ujenzi wa maghala hayo.
Aidha, Wasira aliongeza kuwa ili
kuwa na mafanikio katika sekta ya kilimo nchini, Serikali itapeleka
wataalamu wa matrekta kila mkoa.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo
na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi Zofia Szalczyk alisema kuwa hatua
iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania ni ya muhimu katika katika kuongeza
tija katika uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.
Alisema Poland imefanikiwa
katika sekta ya kilimo kwa sababu inashirikiana na taasisi za kifedha za
kimataifa ambapo ameisifu Tanzania kuchukua uamuzi huo ambao
utaiwezesha kuwa na kilimo chenye tija.
Adha, ameishukuru Serikali ya
Tanzania kupitia Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na Waziri
wa Fedha nchini na kuahidi kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi
hizo mbili katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
No comments
Post a Comment