WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Serikali haikurupuki inapochukua hatua kwa ajili ya jambo fulani kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Lukuvi alisema jana alipokea malalamiko ya wananchi wa wilaya za Temeke na Ilala mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akieleza jinsi ambavyo ofisi yake imemchukulia hatua Ofisa Ardhi Mteule wa Temeke, Godian Mhindi na kumhamishia Bukombe mkoani Geita ambako amekuwa ofisa wa kawaida.
Alisema serikali ilimchukulia hatua Mhindi baada ya kupata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya utendaji wake usioridhisha, kwa kuwa ilielezwa kuwa watendaji wa Temeke mpaka wale wa Ofisi ya Masijala walikuwa na lugha za ovyo.
Waziri huyo alisema baada ya kuchukua hatua hiyo, watu wengi wamekuwa wakiwapigia simu na Naibu Waziri wake, Angela Kairuki, kwamba wamefanya makosa kwa kumhamisha ofisa huyo. “Serikali haikurupuki.
Tangu nimefika nimeambiwa utendaji usioridhisha wa Temeke kwenye masuala ya ardhi. Watu wengi sana wananipigia simu kuwa tumemwonea. “Acheni kuingilia kazi za watu. Tukichukua hatua kama hii kwa ajili ya kuwaponya ninyi msituingilie. Serikali ni yenu itaendelea kuwa yenu, pia ina masikio, na ina macho inaona,” alisema Lukuvi.
No comments
Post a Comment