SERIKALI imelipongeza shirika la Connect Autism Tanzania,kutokana na kusaidiana na serikali katika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum ,yaani Usonji .
Hayo yalielezwa jana na Katibu tawala wa mkoa wa Arusha, Adoh Mapunda, kwenye maadhimisho ya siku ya Usonji, yaliyofanyika viwanja vya Azimio la Arusha.
Kwenye hotuba yake iliyosomwa na Katibu tawala wilaya ya Arusha, Daniel Machunda, Mapunda,alisema serikali imeipa kipaumbele siku hiyo muhimu kutokana na siku hiyo kuwa ni ya kuelimisha umma kuhusu tatizo la Usonji ili kuwezesha jamii kuunganisha nguvu pamoja katika kuwasaidia wenye mahitaji maalum.
Mapunda, alisema Usonji ni tatizo linalotokea katika ukuaji wa mtoto na linaathiri ukuaji wake na linagundulika anapofikia umri wa miaka mitatu na chanzo chake hakijajulikana .
’’Hili tatizo hutokana na upungufu wa kibailojia anaoupata mtoto akiwa tumboni na anapata athari kwenye makuzi yake na kuwa na ulemavu “alisema Mapunda.
Alizipongeza shule ambazo zimekuwa zikiwapokea wanafunzi wenye usonji na kuahidi kuwa serikali itaendelea kulisimamia kikamilifu ili kuhakikisha jamii inaelimishwa na kuwapeleka watoto wenye usonji shuleni wapate elimu ambayo ni haki ya msingi ya kila mtu.
Aidha, Mapunda,aliwapongeza walimu wanaofundisha watoto hao wenye usonji, na wanaowalea kwenye vituo na kueleza kuwa kazi hiyo ya kuwalea na kuwahudumia yataka moyo wa huruma na upendo mkubwa.
Awali mkurugenzi wa shirika la Connects Autism Tanzania, Grace Lyimo,aliishauri serikali kuandaa mtaala wa kuwaendeleza walimu wa elimu maalum baada ya kumaliza vyuo ili kuwepo na wataalamu wa kutosheleza mahitaji kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum.
Alisema kuwa wataalam wanapohitimu mafunzo huwa hakuna mtaala unawaendeleza hivyo wanaiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwepo na mtaala wa kuwaendeleza mara baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Lyimo,akaitaka serikali ianzishe vyuo vya ufundi vinavyokidhi mahitaji maalum ya wanafunzi wenye Usonji ili wanapohitimu elimu ya msingi na sekondari waweze kujiandaa kwa maisha yao ya baadae.
Alisema siku ya Usonji duniani ilianzia nchini Marekani ambapo nchi 138 duniani zikiwemo Afrika kusini, Ghana na Tanzania zinashiriki kwenye maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa April 2 kila mwaka.
Aliongeza kuwa mwaka 2014 siku hiyo iliadhimishwa nchini kwa mara ya kwanza kwenye mikoa miwili ya Kilimanjaro na Dar es Salaam, lakini mwaka 2015 maadhimisho hayo yamefanyika Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam,na mwaka huu yameshirikisha mikoa ya Kilimanjaro Arusha na Dar es Salaam pekee.
No comments
Post a Comment