Mfungaji wa goli la kwanza Amis Tambwe (kushoto) akishangilia na Donald Ngoma baada ya kuifungia Yanga goli la kwanza
Baada ya kusota kwa miaka kadhaa 
hatimaye leo Yanga wamewatuliza watani zao wa Msimbazi Simba kwa 
kuwabanjua kwa goli 2-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara wa 
raundi ya nne ulipigwa kwenye uwanja wa Taifa.
Amis Tambwe na Malimi Busungu 
wameibuka mashujaa kwenye mchezo wa leo lakini sifa pekee zinaenda kwa 
Busungu aliyeingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Msuva na 
kutengeneza bao lililofungwa na Tambwe dakika ya 44 kipindi cha kwanza 
kabla ya yeye kufunga bao la pili dakika ya 79 kipindi cha pili.
Simba watajilaumu wenyewe kwa 
kushindwa kufunga mabao kipindi cha kwanza wakati wanatawala mchezo 
kabla ya mambo hayajawa magumu baadae walipofungwa.
Mpira ulianza kwa kasi huku Simba
 wakitawala sana sehemu kubwa ya mchezo na mara nyingi walitengeneza 
mashambulizi lakini safu ya ushambuliaji iliyokuwa inaongozwa na Hamis 
Kiiza pamoja Mussa Mgosi ilishindwa kutumia nafasi hizo kufunga magoli.
Muda mwingi wa kipindi cha kwanza
 Yanga walikuwa wakishambuliwa huku Simba wakitengeneza mashambulizi yao
 kupitia upande wa winga ya kulia na kumpa Haji Mwinyi kazi ya ziada.
Baada ya kuonekana mchezo 
umemkataa Simon Msuva, kocha wa Yanga alifanya mabadiliko ndani ya 
kipindi cha kwanza kwa kumtoa Msuva na nafasi yake ikachukuliwa na 
Malimi Busungu ambaye alionesha uhai mkubwa na badae kutoa pasi ya goli 
lililofungwa na Amis Tambwe.
Kipindi cha pili mambo yaligeuka 
baada ya Yanga kumiliki mchezo na kufanya mashabulizi kadhaa kwenye 
lango la Simba yaliyokuwa na madhara. 
Wakati Simba wakipambana 
kusawazisha goli walilofungwa kipindi cha kwanza, Malimi Busungu 
alitupia goli la pili na kuzima kabisa matumaini ya kuambulia hata sare 
kwenye mchezo wa leo. 



No comments
Post a Comment