WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamuita Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Bw. Hassan Jarufo ili aje amueleze ni kwa nini wakulima wa zao hilo wanacheleweshewa malipo yao kinyume na maagizo ya Serikali.
Ametoa kauli hiyo jana mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Niliagiza wanunuzi waje na bond (dhamana ya mauzo), waziweke benki ndipo waingizwe kwenye mnada. Kwa maana hiyo mnada ukimalizika, benki inakata fedha husika na kuingiza kwenye chama cha wakulima.”
“Hapa tatizo ni kwamba hatukusimamia vizuri zuala hili. Tulipaswa tujiridhishishe kwanza kama mnunuzi amelipa fedha benki. Tatizo la biashara hii watu wengi ni madalali, wanaangalia hali ikoje na wakibaini kuna cha juu, ndiyo anaagiza na kuamua kuja kulipa. Kama angekuwa amelipa benki, ile hela ya awali ingekatwa katika fedha ya dhamana aliyokwishaitoa,” alisisitiza.
Oktoba 16, 2016 wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine wilayani Nachingwea, mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema alishatoa maelekezo tangu Aprili, mwaka huu kwamba wanunuzi wa korosho ni lazima watoe asilimia 25 ya malipo wanayotaka ili kuepuka tatizo la madalali kuingilia kati biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi na Wakuu wote wa wilaya za mkoa huo wawahimize wakulima wapande miche mipya ya korosho kwa sababu mikorosho iliyopo imezeeka na haitoi mazao ya kutosha.
“Mnatakiwa muwahimize wananchi wapande miche mipya mara tu mvua zitakapoanza ili ianze kukua wakati wakusubiria kung’oa ile ya zamani. Nimeambiwa korosho bora hazipaswi kuzidi punje 190 ili zijae kwenye kilo moja. Ubora wa miti ya korosho ukishuka na idadi ya punje pia inapungua,” alisema.
Alisema kigezo kikuu cha ununuzi wa korosho hivi sasa ni idadi ya punje na kwa Ruangwa na Nachingwea, idadi inakuwa kubwa kwa sababu punje zake ni ndogo. “Wenzetu wa Tandahimba walipanda miche mipya tangu miaka minne iliyopita kwa hiyo sasa hivi wanavuna korosho zenye ubora,” ameongeza.
Alimpongeza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba kwa uamuzi wake wa kuvunja mfuko wa wakfu wa korosho (CIDTF) na akamtaka afute mifuko kama hiyo kwenye mazao mengine kama katani, chai na kahawa kwani inafanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na bodi za mazao hayo.
“Waziri Tizeba alishaanza na zao la pamba, sasa aende kwenye mazao mengine ili fedha ambazo watu wa mfuko huu walikuwa wakizitumia kulipana posho tu, sasa ziende kwenye bodi kuhamasisha wakulima walime zaidi na ikibidi wapewe hata mashine za kupulizia dawa,” aliongeza.
No comments
Post a Comment