Leo ni siku ambayo ilikuwa
ikisubiriwa sana na mashabiki wengi wa soka la Tanzania, leo ndio siku
ambayo unapigwa mtanange wa Dar es Salaam Darby (Yanga vs Simba) mechi
hii inatajwa kuwa miongoni mwa Derby kubwa barani Afrika lakini ikiwa ni
Derby yenye upinzani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Simba na Yanga zinakutana leo
kwenye raundi ya nne ya VPL lakini ikiwa ni mechi ya kwanza
inayozikutanisha timu hizo msimu huu, hapa chini nimekuwekea vitu muhimu
unavyotakiwa kuvijua kabla ya mechi haijapigwa ili wakati wa mchezo
utapofika unakuwa unajua vizuri nini kinaendelea.
Matokeo ya timu zote msimu huu mpaka sasa
Baada ya mechi tatu kuwa
zimechezwa hadi sasa, timu zote zimeshinda michezo yote mitatu Simba
imeshinda mechi zake dhidi ya African Sports na Mgambo JKT ugenini
kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga mechi yao ya tatu walishinda wakiwa
kwenye uwanja wa taifa dhidi ya Kagera Sugar. Yanga mechi zao zote
wameshinda wakiwa kwenye uwanja wa taifa dhidi ya Coatal Union, Tanzania
Prisons na JKT Ruvu.
Vita ya Hamisi Kiiza vs Amis Tambwe
Hawa ni washambuliaji wawili
ambao leo watakuwa wakicheza dhidi ya vilabu vyao vya zamani. Kiiza
alikuwa Yanga kwasasa yupo Simba wakati Tambwe alikuwa Simba na sasa
yupo Yanga na wote kwa pamoja wamekuwa na moto wa ajabu katika kutupia
kambani msimu huu.
Kiiza
Mpaka sasa anaongoza kwa kutupia
nyavuni akiwa amefunga bao tano baada ya kufunga kwenye mechi ya kwanza
bao moja, mechi ya pili bao moja na mechi ya tatu bao tatu na hii ikiwa
ni hat-trick ya kwanza kwa msimu huu lakini ikiwa ni hat-trick yake ya
kwanza pia akiwa Msimbazi.
Tambwe
Amefunga jumla ya bao tatu hadi
sasa. Alifunga bao moja kwenye mechi ya kwanza, halafu mechi ya tatu
akatupia mbili dhidi ya JKT Ruvu wakati Yanga ilipoibuka na ushindi wa
goli 4-1.
Mtiririko wa matokeo
Yanga
Walianza kwa ushindi wa goli 2-0
dhidi ya Coasta Union, wakapata ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Tanzania
Prisons na mechi ya tatu wakashinda kwa goli 4-1 dhidi ya JKT Ruvu. Leo
wanakutana na ‘mnyama’ hii ina maana kama wanaendelea kwa mfululizo huo
wataibuka na goli tano.
Simba
Walianza kwa ushindi wa goli 1-0
dhidi ya African Sports kwenye mechi ya kwanza, mechi ya pili wakashinda
kwa goli 2-0 dhidi ya Mgambo JKT na mechi ya tatu wakaibuka na ushindi
wa goli 3-1 dhidi ya Kagera Sugar. Kama wataendelea na mfululizo huohuo
inamaana leo watafunga bao nne.
Magoli ya kufungwa
Kila timu imeruhusu goli moja
kwenye mchezo wake wa tatu, timu zote zimefungwa kwenye uwanja wa taifa
ambao zinautumia kama uwanja wao wa nyumbani na kila timu imefungwa
kwenye mchezo iliopata ushindi mkubwa.
Yanga
Imefungwa goli moja wakati
ilioibuka na ushindi wa goli 4-1 dhidi ya JKT Ruvu mchezo uliochezwa
kwenye uwanja wa taifa. Yanga wamefunga magoli tisa kwenye mechi tatu
walizocheza.
Simba
Ilifungwa goli moja kwenye
ushindi wake mkubwa msimu huu hadi sasa ilipoifunga Kagera Sugar kwa
goli 3-1 kwenye uwanja wa taifa wakati wao wakiwa wamefunga jumla ya
magoli sita hadi sasa.
Historia ya timu hizo kwenye mchezo wa Dar es Salaam Derby
Timu hizi tayari zimekutana mara
79 kwenye mechi za ligi kuu Tanzania bara, mchezo wa leo utakuwa ni wa
80 huku ukiwa ni wa kwanza kwenye msimu huu wa 2015/16.
Takwimu zinazungumaje?
Mabinwa watetezi wa ligi hiyo
timu ya Yanga wanaongoza kwa kuwafunga watani zao Simba wakiwa
wameshinda mechi 29 kati ya 79 wakati Simba wao wameifunga Yanga kwenye
mechi 23 kati ya 79 huku mechi 27 kati ya 79 zikiwa nisare.
Matokeo ya msimu uliopita
Kwenye mechi ya kwanza msimu
uliopita timu hizo zilitoka sare lakini mechi ya pili (marudiano) Simba
iliitandika Yanga kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Uganda
Emanuel Okwi.
Maswali mawili ya kujiuliza kabla ya mchezo wa leo
1. Je, Yanga ambao ni mabingwa
watetezi wa ligi kuu Tanzania bara watalipa kisasi cha kufungwa mara kwa
mara siku za hivi karibuni au Simba wataendelea kupeleka kilio
Jangwani?
2. Je, ni nani kati ya Kiiza na Tambwe atakaepeleka kilio kwenye timu yake ya zamani?
No comments
Post a Comment