Kiwango cha vifo vya vijana wanaoishi na VVU na Ukimwi kimeongezeka nchini Kenya licha ya kushuka kwa ujumla wa maambukizi ya VVU nchini humo. Utafiti wa hivi karibuni wa shirika la Kenya Aids Survey Indicator (Kasi) na tafiti nyinginezo zilizofanywa na wadau mbalimbali katika sekta ya afya zimethibitisha mwelekeo huo.
Utafiti pia unaonyesha kuwa taasisi nyingi za elimu hazijaweka mfumo madhubuti wa kuwasaidia wanafunzi wanaoishi na VVU.
Wazazi nao wanasemekana kutokuwa wazi na hawazungumzi na walimu na watoa huduma za afya shuleni, kuhusu jinsi wanafunzi walioathiriwa na ugonjwa huo wanavyoweza kuelekezwa namna kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI.
Shirika la kuhudumia watoto la Umoja Mataifa (Unicef) limesema licha ya juhudi kubwa zinazopigwa na wadau mbalimbali katika kupambana na VVU, mkazo hautiliwi kwa vijana ilhali wao ni asilimia 24 ya idadi ya watu Kenya.
Katika Ripoti ya Kenya Aids Survey Indicator, takriban vijana 150,000 walio kati ya umri 10-19 wanaishi na VVU, wakati mara nyingi kampeni huwa zimelenga kwa watoto na watu wazima.
No comments
Post a Comment