picha ikionesha pembe za ndovu{ sio halisi za tukio husika} |
habari kutoka mbeya
SHAHIDI wa Kwanza katika kesi
inayowakabili raia wanne wa Kichina wanaokabiliwa na kesi ya kukamatwa na nyara
za Serikali ikiwa ni Pembe za Faru ameieleza Mahakama jinsi watuhumiwa hao
walivyokutwa na nyara hizo.
Shahidi huyo Godliving Mollel(36)
Afisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Kasumulu wilayani Kyela akiongozwa na
Wakili wa Serikali Archiles Mulisa akisaidiana na Wankyo Saimon mbele ya Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Mbeya, Michael Mteite alisema watuhumiwa hao walikamatwa
Novemba 11, mwaka huu majira ya saa mbili na nusu asubuhi Kasumulu wilayani
kyela.
Shahidi huyo alieleza mahakama kuwa
siku hiyo ya Novemba 11 Raia hao walielekea moja kwa moja katika dirisha la
uhamiaji na baadaye mmoja wao aliyemtambua kwa jina la Song Le alienda kwenye
dawati la Forodha akiomba kupatiwa Hati halisi ya gari kwa kuwa ilibaki wakati
ikipita awali ndipo alipogundua kuwa ni gari iliyoruhusiwa Septemba 26.
Alisema baada ya Raia huyo ambaye
alimtambua kama ndiye mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo alimuomba nyaraka
ili ajiridhishe kama ameingia kihalali nchini na ndipo alipokagua na
kujiridhisha na kumgundua kuwa ndiye aliyekuwa mmiliki wa Gari lililopitishwa
na Zhang Peng.
Alisema wakati akitaka Hati yake ya
gari Mshtakiwa huyo alikuwa na haraka pamoja na wasiwasi jambo ambalo
lilimfanya amtilie shaka na kukumbuka mazingira yaliyopitishiwa gari siku ya
mwanzo.
Mollel alizidi kuiambia Mahakama
kuwa alipokuwa akielekea kwenye Chumba cha kuhifadhia Nyaraka Mshtakiwa alizidi
kumfuata na kumsisitiza kuhusu muda jambo ambalo lilipelekea kupiga Simu kwa
Askari Polisi akimuomba aje ili walifanyie ukaguzi Gari hilo kabla ya
kumkabidhi.
Alisema baada ya kupata Nyaraka
alizokuwa akizihitaji Song le alimsubiri Askari ambaye alipofika walimwamuru
Mshtakiwa kupeleka gari sehemu maalum ya ukaguzi huku akiwa sambamba na Maafisa
wa Uhamiaji, Polisi na Afisa Forodha lakini kabla ya kuanza upekuzi Afisa
Uhamiaji aligundua kuwa wengine hawapo aliofika nao kusaini Pass za kuingilia
nchini.
Alisema baada ya kuwafuata watu hao
ambao ni washtakiwa Xiao Shaodan, Chen Jianlin na Hu Liang ambapo hakuwakuta na
kuamuru kupiga simu Kyela na Tukuyu ili waweze kuzuiliwa endapo watakuwa
wametoroka.
Alisema baada ya dakika 40
washtakiwa walikamatwa wakiwa kwenye gari aina ya Kosta likitokea Kyela
kuelekea Mbeya na baada ya kufikishwa kwenye eneo la ukaguzi upekuzi ulianza
kwa kila mmoja kutoa begi lake na kulishika na ndipo fundi alipoitwa kwa ajili
ya kulifungua gari katika baadhi ya maeneo kwa maelekezo ya askari polisi.
Alisema katika upekuzi huo
waligundua katika buti ya gari mahali ambapo pamechomelewa na kasha kufungiwa
nati kwa chini kama tenki la mafuta na baada ya kulifungua ndipo walipokuta
vitu vimefungwa vinavyodhaniwa kuwa ni pembe za Faru zikiwa 11.
Aliongeza kuwa ndipo aliposaini hati
ya upekuzi ya Polisi kama shahidi wa kwanza na ndipo Maafisa Wanyapori
walipoitwa na kugundua kuwa ni Pembe za Faru zilizokuwa zikitoka Nchini Malawi
na kuingia nchini Tanzania.
Hata hivyo Wakili wa Serikali
alipomaliza kumuongoza shahidi wa Kwanza, Wakili wa Utetezi alimuomba Hakimu
Mkazi Michael Mteite kuahirisha kuendelea kutolewa ushahidi kwa kuwa muda
ulikuwa umeisha na Washtakiwa walipaswa kuwa Gerezani kwa ajili ya Chakula na
Mapumziko.
Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa
Serikali Wankyo Saimon ambaye alidai kuwa kwa mujibu wa makubaliano walipaswa
kupokea ushahidi kutoka kwa mashahidi watano na kesi hiyo ilipaswa kuisha kwa
muda wa siku mbili kutokana na kuwa na mlengo wa kitaifa hivyo akamuomba Hakimu
kuendelea na ushahidi.
Kutokana na Maelezo hayo Hakimu
Mkazi Mteite alikubalina na hoja ya upande wa Utetezi kuwa muda umeisha
kutokana na upande wa mashtaka kutumia muda mrefu wa siku nzima kueleza upande
wao hivyo kuwanyima washtakiwa kuuliza maswali pamoja na wakili wao hivyo
kuamuru kuahirisha kesi hiyo hadi siku inayofuata.
Awali Molel alisema Septemba 26,
mwaka huu mtu mmoja raia wa China aliyefahamika kwa jina la Zhang Peng
akiwa na gari aina ya Toyota Hilux yenye namba za usajili T 103 DER alifika kuomba
kibali kwa ajili ya kwenda nchini Malawi ambapo alipitia taratibu zote ikiwa ni
pamoja na kuonesha vielelezo vyote vinavyotakiwa.
Alisema katika nyaraka alizokuwa
nazo dereva huyoi akabainika kuwa hakuwa mmiliki wa gari wala kuwa na kibali
kutoka kwa mwenye gari jambo ambalo alifuatilia kwa kutumiwa barua kutoka kwa
mmiliki kwa njia ya mtandao kupiti email yake barua iliyotoka kwa mshtakiwa
namba moja Song Lei.
Alisema baada ya kumaliza kupitia
nyaraka zote alimwamuru dereva huyo kupeleka gari eneo maalumu la ukaguzi
ambapo katika upekuzi huo akiwa ameambatana na maafisa wengine walipata
wasiwasi kwenye buti ya hiyo gari baada ya kugundua kuwepo kwa eneo
lililofungwa kwa kutumia nati na kuchomelewa.
Alisema baadaye aliamriwa kufunguliwa
kwa eneo hilo ambapo dereva alikuwa na mtu mmoja ambaye ni raia wa Malawi
alifika na Bisibisi kwa ajili ya kufungua na baada ya kufunguliwa waligundua
kuwepo kwa tenki linguine ndani kiwa limechomelewa kama tenki la kuhifadhia
mafuta lakini baada ya kulipekua pia halikuwa na kitu chochote ndani.
Shahidi huyo aliongeza kuwa baada ya
kujiridhisha na upekuzi huo Dereva huyo aliandikiwa kibali cha muda cha siku
tisini kwa ajili ya kwenda Malawi na kwamba kabla ya hapo walikubaliana kufanya
upekuzi wa kina pindi dereva huyo atakapokuwa akirejea nchini.
No comments
Post a Comment