>>Kubwa ni Uingereza kuamua kushiriki mapambano dhidi ya IS
HABARI: UINGEREZA
Bunge la Uingereza hii leo linatarajia kupiga kura kuiruhusu nchi yao kujiunga na mapambano dhidi ya kundi la dola la kiisilamu la IS nchini Syria.
Waziri mkuu wa Uingereza , David Cameron ambaye ari yake ya kuliangamiza kundi hilo la dola la kiisilamu imeongezeka zaidi hasa baada ya mashambulizi ya mjini Paris anatarajiwa kuongoza mjadala bungeni unaotarajiwa kuchukua zaidi ya saa kumi katika kuelekea upigaji kura huo.
Mawaziri nchi humo wanaimani kwamba wabunge watapiga kura ya ndiyo kuunga mkono hatua hiyo hali ambayo inaashiria kuwa ndege za kijeshi za Uingereza zitaanza mashambulizi kulilenga kundi hilo la dola la kiisilamu huko nchini Syria kabla ya kufikia mwisho wa juma hili.
Cameron amesisitiza ya kuwa hatua za kijeshi zinahitajika sasa ili kuzuia mashambulizi kama yale ya yaliyoua watu 130 mjini Paris mwezi uliopita, lakini pia akiongeza kuwa hatua hiyo itaenda sambamba na juhudi za kidiplomasia zinazoendelea sasa katika kushughulkikia mgogoro wa Syria.
Hata hivyo baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisiasa na ya kivita, wanasema wabunge kadhaa na raia wa kawaida wanaonekana kuwa na mashaka. Makundi ya watu wanaopinga mambo yanayohusiana vita tayari wameandamana kuonyesha kutounga mkono hatua hiyo.
Baadhi ya wachambuzi wanauona hatua hii ya uingereza kutaka kushirika katika kampeni dhidi ya kundi hilo la dola la kiisilamu kama hatua moja wapo ya kuwaunga mkono bega kwa bega washirika wake ambao ni mataifa ya Marekani na Ufaransa.
DWSWAHILI
***************************************************************************
URUSI
Waziri mkuu wa Urusi Bw Dmitry Medvedev amesaini amri ya serikali ikibanisha vikwazo vitakavyowekwa dhidi ya Uturuki.
Vikwazo hivyo vitakavyofanya kazi kuanzia tarehe mosi, Januari mwakani ni pamoja na kusitisha kusamehe visa kwa waturuki wanaoingia Urusi wakiwa na pasipoti ya kawaida, kupiga marufuku ya kuagiza mboga, matunda, nyama za ndege na chumvi kutoka Uturuki, na kupunguza idadi ya ruhusa hadi kuwa chini ya elfu 2 kwa makampuni ya usafirishaji wa magari ya Uturuki kusafirisha bidhaa nchini Urusi.
Amri hiyo pia imesema, kuanzia leo, Russia itapiga marufuku safari za ndege za kukodi kati ya Uturuki na Urusi, kusitisha miradi ya uwekezaji wa kibiashara na mikutano ya uwekezaji wa biashara kati ya serikali za nchi hizo, kusitisha uanzishaji wa mfuko wa pamoja wa uwekezaji na shughuli za kamati ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili.
Pia imesema, Urusi itasimamisha ushirikiano wa sekta za sayansi na utamaduni kati yake na Uturuki kuanzia mwaka kesho hadi mwaka 2019.
Bw. Medvedev amesema, serikali ya Urusi itaongeza vikwazo dhidi ya Uturuki kama ikihitajika.
&& CRI &&
************************************************************
AFRIKA KUSINI
Waafrika wengi wanasema kuwa ufisadi umeongezeka
katika kipindi cha miezi 12 iliyopita na serikali nyingi za bara hilo
zikionekana kushindwa kukomesha rushwa na miamala ya siri ya ufisadi.
Hayo
yameelezwa na Taasisi ya Transparency International kupitia uchunguzi wake wa
maoni.
Katika uchunguzi huo wa maoni, Afrika Kusini
imetajwa kuwa nchi inayoongoza kwa ufisadi barani Afrika ikifuatiwa na Ghana na
Nigeria.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema mwezi
Oktoba kwamba chama tawala nchini humo kimekuwa kikipoteza uungaji
mkono wa wananchi kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa
mwakaani, kutokana na kuwa chama hicho kimekuwa hakiwachukulii hatua kali
mafisadi.
Transparency International imewasilisha uchunguzi
huo wa maoni katika kipindi hiki ambapo nchi nyingi za Kiafrika
zinakabiliwa na mashinikizo ya wananchi na ya vyama vya upinzani, kufuatia
kushindwa serikali kupambana na ufisadi wa mali ya umma kwa kushindwa
kuwafungulia mashtaka maafisa wote wa ngazi za juu serikalini wanaohusika na
kashfa za ufisadi.
&& BBCSWAHILI &&
*****************************************************
Libya
Ndege za kivita za Libya zimezishambulia ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ambalo limekuwa likifanya kila liwezalo kupanua udhibiti wake katika maeneo yenye mafuta mashariki mwa nchi hiyo.
Ndege za kivita za serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa jana ziliishambulia nyumba moja katika eneo la viwanda la mji wa Ajdabiya, ambako magaidi wa Daesh walikuwa wakifanya mkutano.
Shambulio hilo la anga ni katika muendelezo wa mashambulizi kadhaa yaliyofanywa na Libya wiki iliyopita, katika kile kilichotajwa na serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa kuwa ni sehemu ya oparesheni zake dhidi ya ugaidi zenye lengo la kuwazuia magaidi wa Daesh kuuteka mji wa Ajdabiya ambao sasa upo mikononi mwa wapiganaji watiifu kwa serikali hiyo.
&& CRI &&
*******************************************************
PARIS UFARANSA
Nchi za Kiafrika zimesisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua madhubuti ili kupata ufumbuzi wa ongezeko la hali ya joto duniani.
Wakuu wa nchi kadhaa wa Kiafrika ikiwemo Senegal, Cameroon, Zimbabwe, Gabon na Djibouti wamebainisha kuwa nchi zote zinapasa kustafidi na fursa iliyopo ili kuzuia kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi duniani.
Viongozi hao wameyaeleza hayo pambizoni mwa kikao cha mabadiliko ya tabianchi mjini Paris Ufaransa.
Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ameeleza kuwa, miaka 50 imepita hadi sasa ambapo hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa na kwamba kuendelea kwa hali hii ya sasa na kuongezeka kwa hali ya joto, kutayafanya maisha ya watu katika maeneo kama Mashariki ya Kati na Afrika kuwa ya mashaka zaidi kuliko huko nyuma.
Naye Rais Ali Bongo wa Gabon amesema, Afrika ni mhanga wa kwanza wa athari za mabadiliko ya tabianchi, huku nchi za bara hili zikikabiliwa pia na tatizo la usambazaji wa teknolojia ya kisasa na gharama zake.
Ukame endelevu, mafuriko, ukosefu wa mvua na kupungua kwa maeneo ya kilimo ni baadhi tu ya taathira za mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.
&& IRIBSWAHILI &&
*********************************************************
UJERUMAN
Bunge la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,Bundestag linaanza kuujadili hii leo mpango wa kujiunga wanajeshi wa Ujerumani na juhudi za kuwapiga vita wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam-IS nchini Syria.
Baada ya baraza la mawaziri kupitisha uamuzi huo,bunge la shirikisho linatazamiwa kuuidhinisha hadi ifikapo mwisho wa wiki hii.
Mpango huo unategemewa kuidhinishwa kutokana na wingi wa kura za wabunge wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano- CDU/CSU na SPD.
Wawakilishi wengi wa makundi ya vyama hivyo wameonyesha azma ya kuunga mkono mpango wa kutumwa wanajeshi wa Ujerumani kupambana na IS.
Makundi ya vyama vya upinzani vya die Linke na walinzi wa mazingira die Grüne wanapanga kuupinga mpango huo.
Serikali kuu inapanga kutuma wanajeshi 1200,ndege za upelelezi na za kutia mafuta pamoja na manuari kuisaidia manuari ya Ufaransa inayobeba ndege za kijeshi "Charles de Gaule" iliyoko karibu na fukwe za Syria.
Kwa mujibu wa wizara ya ulinzi mjini Berlin, wanajeshi wa Ujerumani wanaweza kuanza kupelekwa katika eneo hilo wiki ijayo.
&& DWSWAHILI &&
****************************************************************************
No comments
Post a Comment