SYRIA
Maelfu ya waasi ambao walitarajiwa
kusaidiwa kuondoka kutoka kambi ya wakimbizi ya Yarmouk na maeneo ya
karibu hawakuondoka kama ilivyotarajiwa, ripoti zinasema.
Wapiganaji hao na familia zao walikuwa wamepangiwa kusafirishwa kutoka kambi hiyo kusini mwa Damascus hadi maeneo yanayodhibitiwa na makundi yao, chini ya mkataba kati ya serikali na waasi.
Takriban raia 18,000 wamekwama Yarmouk kutokana na mapigano na kuzingirwa na vikosi vya serikali tangu 2012.
Wapiganaji wa Islamic State (IS) walitwaa udhibiti wa baadhi ya maeneo ya kambi hiyo mapema mwaka huu.
Lakini walifurushwa na wapiganaji wa Kipalestina na wapiganaji wengine wa Syria baada ya mapigano makali.
Tangu wakati huo, kambi ya Yarmouk imekuwa imegawanywa kwa maeneo yanayodhibitiwa na IS, kundi la al-Nusra Front lenye uhusiano na al-Qaeda na wapiganaji wa Kipalestina wanaounga mkono na wanaopinga serikali.
Wanajeshi wa serikali wameweka vizuizi kuzingira eneo hilo na huzuia raia kuondoka.
Chini ya makubaliano ya sasa, wapiganaji hao walitarajiwa kuruhusiwa kuondoka Yarmouk na maeneo jirani ya Hajar al-Aswad na al-Qadam.
Mabasi 18 tayari yalikuwa yamewasili eneo hilo Ijumaa kuwasafirisha.
Runinga ya kundi la Hezbollah la Lebanon kwa jina al-Manar imesema mpango wa kuwahamisha umeahirishwa kwa sababu msafara wao ungepitia maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Jaysh al-Islam, ambalo kongozi wake aliuawa baadaye Ijumaa.
Kambi ya wakimbizi ya Yarmouk ilijengwa kwa ajili ya Wapalestina waliokuwa wakitoroka vita vya Waarabu na Waisraeli vya 1948. Kabla ya vita kuanza Syria 2011, ilikuwa na wakimbizi 150,000.
BBCSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
UFARANSA
Kundi la watu limevamia na kuharibu
ukumbi wa maombi wa Waislamu katika kisiwa cha Ufaransa cha Corsica
katika kinachoonekana kuwa shambulio la kulipiza kisasi kushambuliwa kwa
wazima moto kisiwani humo.
Mamia ya watu walikuwa wamekusanyika katika mji huo mkuu kulalamikia kujeruhiwa kwa wazima moto wawili na afisa mmoja wa polisi Alhamisi.
Watatu hao walishambuliwa na vijana waliokuwa wamejifunika nyuso.
Serikali imeshutumu visa vyote viwili na kuahidi kuadhibu waliohusika.
Shirika la habari la AFP linasema baadhi ya waandamanaji walienda hadi eneo ambapo maafisa hao walishambuliwa na kuanza kuimba “Waarabu waondoke!” na “Hapa ni nyumbani.”
Baadaye, walishambulia ukumbi wa maombi wa Waislamu, wakapora na kuchoma kiasi baadhi ya vitabu, zikiwemo nakala za Koran.
Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls ametaja shambulio hilo kuwa “lisilokubalika”.
Baraza la Waislamu la Ufaransa pia limeshutumu ghasia hizo.
Ufaransa imeimarisha usalama wakati huu wa sikukuu ya Krismasi baada ya shambulio la 13 Novemba kusababisha vifo vya watu 130.
BBCSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
UTURUKI
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
alimshawishi mwanamume, aliyetaka kujiua kwa kujirusha kutoka kwa
daraja, kubadilisha nia yake na kutojiua, afisi yake imesema.
Msafara wa magari ya Bw Erdogan ulikuwa unapita kwenye daraja hilo mjini Istanbul wakati huo.
Picha zilizoonyeshwa kwenye televisheni zilionyesha wahudumu wa Bw Erdogan wakimsihi mwanamume huyo aliyekuwa akitokwa na machozi kuzungumza na rais.
Mwanamume huyo alitembea hadi kwenye gari la rais huyo na wakazungumza.
Baada ya muda mfupi, alisindikizwa kutoka eneo hilo.
Mwanamume huyo alikuwa akitatizwa na msongo wa mawazo kutokana na matatizo ya kifamilia, na polisi walikuwa wamejaribu kumzuia asijirushe kwa saa mbili bila mafanikio, shirika la habari la Dogan limeripoti.
Afisa wa afisi ya rais huyo ameambia shirika la habari la Associated Press kwamba kiongozi huyo aliahidi kumsaidia.
BBCSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
IRAQ
Majeshi ya Iraq yamesonga ndani kabisa ya eneo lililosalia lilalodhibitiwa na wapiganaji wa Dola la Kiislamu katika mji wa Ramadi.
Kuukomboa mji wa Ramadi, ambao uliotekwa na kundi la IS mwezi Mei, utakuwa ni ushindi muhimu wa karibuni kwa majeshi ya Iraq tangu IS ilipoyakamata maeneo mengi ya nchi hiyo mwaka wa 2014.
Msemaji wa jeshi la Iraq linaloendesha operesheni hiyo Brigedia Yahya Rasool amesema wanajeshi waliingia usiku wa kuamkia leo katika kitongoji cha Hoz ambacho ni makao makuu ya ofisi za serikali ya mkoa.
Amesema mashambulizi ya anga yalisaidia kuliyapua mabomu yaliyokuwa yametegwa kwenye majumba, na kuyawezesha majeshi ya serikali kusonga mbele.
Hata hivyo bado ni vigumu kuthibitisha ripoti zinazotoka mjini humo.
DWSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
BURUNDI
Wafuasi wanaoiunga mkono serikali leo wameandamana kote nchini Burundi kupinga mipango ya Umoja wa Afrika kutuma wanajeshi 5,000 wa kulinda amani nchini humo.
Maandamano hayo yamefanyikka kwenye miji mikubwa ilioko katika majimbo 18 ambapo waandamanaji mjini Bujumbura walikuwa na mabango yenye kusema "Tunapinga kutumwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Burundi" na "Hakuna vita au mauaji ya kimbari kuhalalisha kuletwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika".
Makamu wa Rais Gaston Sindimwo akizungumza katika maandamano ya mjini Bujumbura amesema "Hakuna askari wa kigeni akayekanyaga ardhi ya Burundi bila ya idhini ya serikali."
Umoja wa Afrika umesema kikosi cha awali kilichopangwa kutumwa nchini humo kitakuwa na mamlaka ya kuzuwiya vitendo vyoyote vinavyofanya hali ya usalama kuzidi kuwa mbaya na kuchangia kuwalinda raia walioko hatarini.
Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika limesema iwapo Burundi haitokubali kutumwa vikosi hivyo nchini humo katika kipindi kisichozidi saa 96, wanajeshi hao wa kulinda amani watatumwa nchini humo kwa itakavokuwa hata kinyume na matakwa ya serikali ya nchi hiyo.
DWSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
UJERUMAN
Uchunguzi mpya unaonyesha kuwa ni asilimia 16 tu ya Wajerumani wanahisi kuwa nchi yao imenufaika na hatua ya mwaka huu ya kuwakaribisha waomba hifadhi wanaomiminika nchini humu.
Kwa mujibu wa mtafiti Horst Opaschowski, asilimia 16 ya watu walielezea matumaini kuwa mmininiko wa wakimbizi utatoa fursa zaidi za kiuchumi badala ya matatizo katika taifa hili.
Suali jingine lililoulizwa ni ikiwa hatua ya kuwakaribisha wakimbizi wengi inaweza kuimarisha taswira ya Ujerumani kote ulimwenguni.
Ni asilimia 12 tu ya raia waliokubali kutoka upande wa mashariki ambao unakabiliwa na matatizo mengi kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi, ambapo inatarajiwa kufika milioni moja mwaka huu.
Kwa upande wa magharibi waliokubali ni asilimia 22.
DWSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
UTURUKI
Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu ameufuta mkutano uliokuwa umepangwa na chama kinachounga mkono Wakurdi cha People's Democratic - HDP, akisema kuwa siasa zake zimekita mizizi katika machafuko.
Hatua hiyo inakuja wakati majeshi ya serikali yakiendelea na operesheni kali katika upande wa kaskazini mashariki mwa nchi ulio na Wakurdi wengi.
Davutoglu alitarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vyote vitatu vya upinzani bungeni ili kujadili mageuzi yanayopendekezwa ya katiba.
Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu imesema kauli za karibuni za maafisa wa chama cha HDP zinaashiria siasa zinazotokana na vurugu na hofu kwa hiyo hakuna haja ya kukaa kwenye meza moja na watu walio na mtazamo wa aina hiyo.
DWSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
CAR
Jamhuri ya Afrika ya Kati itaandaa uchaguzi muhimu Jumatatu wiki ijayo wakati kukiwa na ulinzi mkali, ikitarajia kufungua ukurasa mpya kutokana na machafuko ya kidini yaliyoikumba nchi hiyo.
Uchaguzi huo uliocheleweshwa wa rais na wabunge unafuatia kura ya maoni ya Desemba 13 ambayo iliidhinisha kwa asilimia 93 katiba mpya, kuonyesha kuwa raia wana shauku nchi hiyo kurejea katika hali ya utulivu.
Katiba hiyo mpya, inauwekea kikomo muhula wa rais hadi miaka miwili na kuweka hatua kali dhidi ya makundi ya wapiganaji wenye silaha ambayo yanajipenyeza katika maeneo makubwa ya nchi hiyo.
Kuna wagombea 30 wanaowania kiti cha urais, akiwemo mtoto wa kiongozi aliyejiita mfalme Jean-Bedel Bokassa. Wengine ni Anicet Georges Dologuele, waziri mkuu wa zamani anayefahamika kama "Bwana Safi" kutokana na juhudi zake za kuangamiza rushwa na wizi.
DWSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
IRAQ
Takribani wagombea 12,000 wamejiandikisha kushiriki katika uchaguzi wa wabunge nchini Iran mwezi Februari mwakani, na kuvunja rekodi za ushiriki katika wakati ambapo kuna hali ya sintofahamu ya kisiasa katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Rais Hassan Rouhani, wa siasa za wastani za mrengo wa kati ambaye alishinda uchaguzi kwa wingi wa kura mwaka wa 2013 na kuunga mkono juhudi za kufikia mkataba wa nyuklia mwezi Julai na mataifa yenye nguvu duniani, anataraji kuwa wafuasi wake wanaweza kuchukua udhibiti wa bunge lenye viti 290 na kumaliza miaka mingi ya udhibiti wa bunge wa wanasiasa wa kihafidhina.
Kwa kupata viti vingi, kutampa Rouhani mamlaka makubwa ya kushinikiza mageuzi ya ndani ya nchi na kuimarisha uhuru wa kijamii na kisiasa - nyanja ambayo hadi sasa juhudi zake zimekuwa zikikaguliwa na mfumo wa mahakama na vikosi vya usalama.
DWSWAHILI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
No comments
Post a Comment