Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad jana aliwasili Zanzibar
kutoka ughaibuni na kulilaumu Jeshi la Polisi nchini akisema, “hapana
shaka yoyote sasa limegeuka tawi la CCM.”
Maalim Seif alisema
hayo jana jioni wakati akizungumza na wafuasi wake waliofika kumpokea
katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume na baadaye kumsindikiza
hadi nyumbani kwake Mbweni mjini hapa.
Baadhi ya viongozi wa CUF
waliohudhuria mapokezi hayo ni pamoja na Mansour Yussuf Himid, Nassor
Ahmed Mazrui, Fatma Abdulhabibi Ferej na aliyekuwa mgombea mwenza wa
Chadema chini ya mwavuliwa wa Ukawa katika urais wa Muungano, Juma Duni
Haji.
Maalim Seif aliyetokea India kupitia Falme za Kiarabu,
alisema anaunga mkono kauli za Mazrui ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wake,
zilizosababisha ahojiwe na polisi juzi, kuwa “sasa CUF wamechoka na
uhuni dhidi ya mali na ofisi zao.”
“Nasikitika kuona hujuma,
watu wakipigwa na kujeruhiwa na mazombi kila kukicha, polisi wapo
wanayaona na hakuna aliyeitwa kuhojiwa kwa uchochezi. Sasa haitawezekana
na haitakubalika tena...” alisema.
Alipoulizwa kuhusu madai
hayo jana, Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu alimtaka mwandishi
kuzungumza na msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba ambaye simu yake
haikupatikana.
Hata hivyo, akizungumzia suala la mazombi hivi
karibuni, Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar, Salum Msangi alisema taswira
ya haraka wanayoipata ni kwamba inawezekana wanaotendewa vitendo hivyo
ni wahalifu ambao wamekutana na wahalifu wenzao hivyo kuhofia kutoa
taarifa ili uhalifu wao usibainike hali inayosababisha kunung’unika
pembeni bila ya kufikisha taarifa maeneo sahihi ili zifanyiwe kazi.
“Kwa
mujibu wa taratibu zilizopo ni kwamba mtu yeyote anayefanyiwa kitendo
cha kihalifu anapaswa kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi ili hatua za
uchunguzi au upelelezi zifanyike ili kubaini wahalifu hao,” alisema
Msangi.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif alimlaumu, Dk Ali Mohamed Shein kuwa si muungwana akidai kuwa amekataa kuondoka madarakani.
Alisema
la kushangaza zaidi ni kuona aking’ang’ania uchaguzi wa marudio,
ilihali hakuna mantiki wala kifungu chochote cha sheria kinachohalalisha
hatua hiyo.
“Nasema sisi hatutambui uchaguzi huo wa marudio
maana wameshindwa kututhibitishia ni wapi zilipo hizo dosari za uchaguzi
uliokwishafanyika,” alisema.
Katika salamu hizo za takriban
dakika 10, Maalim Seif alimtahadharisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha asijaribu kulazimisha chama hicho
kushiriki uchaguzi ‘batili’ wa marudio.
No comments
Post a Comment