Meneja Mkuu wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Glory Farm & Agricultural Products, Justin Nyamoga akitoa maelezo jinsi kiwanda hicho kinavyofanya kazi zake kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) aliyeambatana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo (kushoto), Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la UNFPA, Dk. Hashina Begum (kulia) pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la FAO nchini, Patric Otto kukagua miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa mjini Dodoma. (Picha na Modewjiblog).
Na Mwandishi wetu
Kutoratibiwa kwa mbegu za alizeti na ukosefu wa mitaji umeelezwa kuwa changamoto kubwa kwa wasindikaji wadogo wa mafuta ya mbegu ya alizeti katika kuendesha viwanda vyao kwa gharama nafuu.
Hayo yameelezwa na Wakala wa uendelezaji Kongano la Mafuta ya Alizeti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Viwanda (UNIDO) Vedastus Timothy wakati akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez.
Mratibu huyo alikuwa Dodoma kwa shughuli mbalimbali za ukaguzi wa miradi pamoja na kuhudhuria shughuli za bunge la Tanzania lililomalizika jana.
Timothy alisema kwamba pamoja kuwepo kwa taarifa za kuwepo kwa mbegu za kutosha nchini Tanzania,hali halisi inayoelezwa na wasindikaji inaashiria kwamba sekta hairatibiwi vyema kwani wasindikaji hukaa muda mrefu bila kuwa na mbegu za kusindika.
Aidha alisema kwamba mbegu za alizeti zinazovunwa kuanzia Aprili hadi Julai na huwa na bei nafuu kipindi hicho lakini kama wasindikaji wakikosa mitaji na kununua mbegu chache, msimu unapoisha hawawezi tena kuendelea kufungua viwanda vyao.
Alisema kwamba wasindikaji hao wanakumbana na kiwango kikubwa cha riba kuanzia asilimia 20 kwenda juu , riba ambayo inakwamisha maendeleo ya viwanda hivyo.
Hata hivyo alipoulizwa wanafanya nini katika kusaidia wasindikaji hao kukabiliana na hali hiyo alisema kwamba kupitia kongano hilo na Shirikisho la wasindikaji wadogo wa alizeti kanda ya mashariki na kati (CEZOSOPA). wana mipango ya kuwezesha wasindikaji hao kuwa na nguvu katika soko na kuwa na uwezo wa kupata mitaji bila gharama kubwa.
Aidha kupitia kongano hilo chama hicho kitawezeshwa uboreshwaji wa viwanda vya wanachama wake ili viweze kushindana na kukidhi viwango vya Shirika la Viwango nchini Tanzania (TBS).
Wakala huyo alisema hayo katika mahojiano yaliyofanyika kufuatia ziara ya mradi wa Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez kwenye kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Glory Farm & Agricultural Products kilichopo katika kijiji cha Nzuguni, manispaa ya Dodoma, kinachonufaika na mradi wa ubia wa uboreshaji viwanda kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) na Wizara ya Viwanda na Biashara (TIUMP).
Kwa mujibu wa taarifa ya UNIDO, taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inachangia kuimarika kwa sekta ya viwanda vidogo na vya kati vya usindikaji mafuta na kuviweka katika ushindani.
Aidha kupitia UNIDO ni viwanda hivyo vinawekwa katika hali ya kukua kuwa viwanda vikubwa.
Katika ushirika wa aina hiyo ni matarajio ya mradi huo kufanikisha juhudi za kupunguza umaskini kama moja ya malengo ya maendeleo endelevu yanayotarajiwa na dunia.
Aidha katika upunguzaji huo wa umaskini mradi utachangia ongezeko la fursa za ajira na ukuaji wa uchumi.
Mkoa wa Dodoma wenye viwanda vya kusindika mbegu za alizeti vinavyofanyakazi katika mkaazi wakitumia zana dhaifu na vifungashia visivyokuwa na ishara yoyote ile na kuuza bidhaa zao kando mwa barabara wanahitaji mfumo thabiti wa ukuzaji wa shughuli zao na kueleweka.
Kutokana na mazingira hayo wajasirimali hawa hujikuta wakiingia hasara kubwa kwa kupoteza tija na pia soko lenye uhakika.
Kutokana na madhara hayo na pia kukosa hati ya ubora kwa kukosa mazingira yanayoruhusu hati hiyo kutolewa, TIUMP imelenga kusaidia wasindikaji hawa na teknolojia sahihi inayohitajika ili watoke pale walipo na kuwa na viwanda vidogo au vya kati.
Ingawa kwa sasa UNIDO inasaidia viwanda vinane vya mbegu za alizeti ili kuweza kuboresha bidhaa zao na utendaji kuna muonekano wa maendeleo makubwa siku za usoni hasa kwa wanachama wa CEZOSOPA ambao wameuinganishwa pamoja kwa ajili ya misaada mbalimbali ya kuwawezesha kuwa washindani katika soko.
UNIDO wanatumia maarifa waliyojifunza Ethiopia kuimarisha wanachama wa CEZOSOPA ambao tayari wamekubali kuunda kampuni ya pamoja na kuwekeza katika kitu wanachokifanya kwa pamoja kwa lengo la kuongeza uwezo na ushindani katika soko.
Halmashauri ya Chamwino tayari imekubali kuipa ardhi CEZOSOPA kwa ajili ya uwekezaji huo mkubwa.
Aidha UNIDO imewezesha kupatikana kwa teknolojia rahisi kwa ajili ya usafishaji wa mafuta ya alizeti na teknolojia hiyo inafanyiwa kazi na VETA.
UNIDO wamesema teknolojia hiyo hiyo inasaidia kuweka mafuta katika viwango vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa na kwamba teknolojia hiyo tayari inafanyakazi nchini katika viwanda viwili na vingine saba vimeonesha nia ya kupata teknolojia hiyo.
Imeelezwa kuwa fedha za mradi huo zinapatikana kutoka UNIDO na wadau wengine kama SIDA na UNDAP.
No comments
Post a Comment