Mgombea urais wa chama cha
Republican nchini Marekani Donald Trump ameahidi kumaliza uhalifu na
ghasia nchini Marekani iwapo atachaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu
mwezi Novemba.
Aidha, ameahidi kuchukua hatua kali kukabiliana na wahamiaji haramu na akaonga kuwa kwa sasa wahamiaji wanaruhusiwa kuingia na kuishi katika jamii za Marekani bila kuzingatia usalama wa umma.
Bw Trump amejieleza kama mkombozi na sauti ya wanyonge na watu waliosahaulika nchini Marekani, na akajionyesha kama mtu mwenye sifa tofauti na mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton ambaye sana amemuonesha kama mtu mfisadi na asiyewajibika.
Mfanyabiashara huyo tajiri kutoka Marekani amesema atakomesha sera ya kujenga mataifa na kufanikisha mageuzi ya serikali katika nchi nyingine ambayo amesema imefeli.
Amesema sera hiyo ndiyo chanzo cha matatizo yanayoshuhudiwa nchini Iraq, Libya, Misri na Syria.
Ameahidi kufanya kazi na washirika wote wa Marekani wanaotaka kuangamiza kundi la Islamic State.
Ameituhumu Uchina kwa wizi wa haki miliki za Wamarekani, na kuieleza Beijing kama taifa lililohadaa zaidi katika thamani ya sarafu yake katika historia.
Bw Trump ameahidi kushauriana upya na washirika kuhusu mikataba ya kibiashara kuhakikisha Marekani inafaidi.
No comments
Post a Comment