Mwanamuziki mkongwe, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele ameeleza sababu zilizopelekea jana kutangaza kung’atuka ndani ya Chama Cha ACT – Wazalendo mwaka mmoja baada ya harakati za uchaguzi Mkuu ambao aliutumia kugombea ubunge wa Morogoro Mjini.
Afande Sele ameeleza kuwa moja kati ya sababu zilizopelekea yeye kung’atuka ni kutofikia malengo yake ya kuingia ndani ya chama hicho ya kupata ubunge.
“Nimejitoa ACT- Wazalendo kwa makusudi kabisa na hili lilikuwa ni jambo tarajiwa, kitu cha kwanza moja ya matarajio yalikuwa baada ya mimi kuingia ACT nakuwa Mbunge ila sasa sikupata Ubunge na kama ningeupata Ubunge basi nisingejitoa ndani ya chama,” Anasema Afande Sele .
Jana, kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwanamuziki huyo alieleza kuwa amechukua uamuzi huo sio kwa bahati mbaya hivyo uamuzi wake uheshimiwe. Alisisitiza kuwa hatajiunga na chama chochote cha siasa hadi pale ambapo ataamua vinginevyo.
Mei mwaka jana, Afande Sele alitangaza kugombea ubunge wa Morogoro mjini kupitia ACT-Wazalendo lakini hakufanikiwa kuupata ubunge wa jimbo hilo kupitia sanduku la kura, Oktoba 25 mwaka jana.
No comments
Post a Comment