Na John Banda, Dodoma
WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI)George Simbachawene amemvua cheo cha Ukurugenzi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Agustino Kalinga kwa kushindwa kuwasimia watumishi waliopo chini yake.
Pia Waziri huyo amemsimamisha kazi Ofisa elimu vifaa na takwimu msingi wa manispaa hiyo Josephine Akimu kwa kosa la kudharau maelekezo ya kiongozi wake kwa kusaini barua kwa niaba ya Mkurugenzi huku akitumia jina la Afisa elimu wake bila ridhaa yake.
Hatua hiyo ilitangazwa jana mjini hapa na Waziri Simbachawene wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Waziri huyo alisema kuwa kutokana na kubainika kwa kasoro katika Shule ya msingi Dodoma Makulu ya kuandikwa kwa barua toka ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ikielekeza uchangishwaji fedha kwa wazazi wa michango ya maji,umeme na mlinzi michango ambayo ilishafutwa na Serikali.
“Mkurugenzi huyu wa Manispaa ya Dodoma Kalinga ameshindwa kuwasimamia watumishi walio chini yake hadi kusababisha kuandikwa na kusambazwa barua kwa walimu wakuu wa shule za msingi Manispaa ya Dodoma ambayo inatofautiana na maelekezo ya serikali yaliyopo kwenye mwongozo,”alisema
Pia alisisitiza kuwa Mkurugenzi huyo ameshindwa kusimamia utekelezaji wa maelekezo sahihi ya serikali kuhusu utoaji wa elimu msingi bila malipo hivyo namvua cheo hicho ili hatua nyingine ziweze kuchukuliwa .
Aidha Waziri huyo amempa onyo Ofisa wa elimu msingi wa Manispaa ya Dodoma Scola Kapinga kwa kosa la kutokuwa makini na idara yake hadi kusababisha barua hiyo kuandikwa na kupelekwa shuleni bila yeye kuwa na taarifa.
“Nawaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa kuendelea kuwaelimisha wakuu wa shule za msingi na sekondari katika maeneo yao kuhusu utoaji wa elimu bure bila malipo.
Wiki iliyopita Waziri George Simbachawene akiambatana na Naibu katibu mkuu Tamisemi elimu,Bernard Makali alifanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya msingi Dodoma Makulu kujionea hali halisi ya mgawanyo wa fedha za elimu bure na kubaini barua toka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma iliyoandikwa na Ofisa elimu msingi kuelekeza michango ya fedha za maji,umeme na mlinzi kwa wazazi.
Imeandaliwa na John Banda
Imehaririwa na Denice J. Kazenzele
January 25/2016
No comments
Post a Comment