Baada ya kuanzisha mashambulizi ya angani nchini Syria, Urusi imetoa
wito kwa dunia kuungana katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, na
imesambaza andiko la muswada wa azimio la UN kusaidia kufanikisha azma
hiyo.
Waziri Lavrov alisema yeye na waziri Kerry bado wanatofautiana kimtazamo kuhusu suluhu ya mgogoro wa Syria lakini wamekubaliana kutafuta njia za kuanza mchakato wa kisiasa. "Sote tunataka Syria inayofuata demokrasia, iliyoungana, isiyoegemea dini na ambayo ni nyumbani kwa makundi yote ya kikabila na kiimani ambayo haki zake zinalindwa, lakini tunatofautiana juu ya namna ya kufika huko. Lakini tumekubliana juu ya baadhi ya hatua za kuweka mazingira ya kuwezesha mchakato wa kisisasa," alisema Lavrov.
Syria yaiunga mkono Urusi
Moja ya shambulizi lililofanywa na ndege za Urusi nchini Syria.
Muswada wa Urusi unayatolewa mwito mataifa kuratibu shughuli zao kwa ridhaa ya serikali za mataifa katika eneo zinakofanyika shughuli hizo. Lugha ya muswada huo, ambayo inamaanisha serikali ya Syria, inafanana na ile iliyotumika katika muswada wa awali wa taarifa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa na Urusi lakini Marekani ikakataa kuujadili.
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Wallid al Muallem aliliambia baraza la usalama kuwa nchi yake inaridhia kwa dhati hatua za Urusi na kuyaita mashambulizi ya Ufaransa na mengine nchini Syria yasiyoihusisha serikali yake kuwa ukiukaji wa dhahiri wa sheria za kimataifa.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif , mshirika wa karibu zaidi wa utawala mjini Damascus, alibainisha kuwa muungano unaoongozwa na Marekani ulikuwa unashindwa kufikia malengo yake.
Marekani kuzungumza na Urusi
Waziri Lavrov alisema Urusi iko tayari kuweka njia za kudumu za mawasiliano kuhakikisha mapambano hayo yanafanikiwa.
Alizitaja nchi zenye dhima kubwa katika kutatua mgogoro wa Syria zikiwemo Iran, Urusi, Saudi Arabia, Uturuki, Misri, Jordan, Qatar, Marekani na hata China. Alisema wanachokihitaji ni mikakati ya pamoja inayoungwa mkono na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Waziri John Kerry alisema Marekani iko tayari kufanya kile alichokiita mazungumzo ya kuondoa mgogoro na Urusi kuhusiana na kampeni mbili za mashambulizi haraka iwezekanavyo. "Tumekubaliana hata kama bado hatujapata azimio kuhusiana na chaguo muhimu katika suluhu ya kisiasa, kwamba kuna hatua makhsusi zinazoweza kusaidia kutuongoza katika mwelekeo sahihi."
Balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa Abdallah Al-Mouallimi, aliyatuhumu mashambulizi ya Urusi kwa kulenga maeneo ambako hakuna wapiganaji wa Daesh au Dola la Kiislamu, na kusababisha vifo vya raia wasiyo na hatia -- tuhuma ambazo hata hivyo zimekanushwa na waziri Sergei Lavrov.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius, ambaye nchi yake ilianzisha mashambulizi ndani ya Syria siku chache zilizopita, aliliambia baraza kuwa Ufaransa iko tayari kushirkiana na Urusi kwa masharti ya kukomesha vurugu dhidi ya raia wa Syria, waweke bayana kabisaa nani mataifa yanapambana naye na kuondoka kwa rais Bashar al Assad-
No comments
Post a Comment