Timu za Yanga na Azam zimeshindwa
kutambiana kwa mara nyingine tena baada ya kulazimishana sare ya
kufungana goli 1-1 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara
uliochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ndio walikuwa wa kwanza
kupata goli dakika ya 45 kipindi cha kwanza mfungaji akiwa ni
mshambuliaji wao tegemezi Donald Ngoma ambaye alifunga goli hilo kwa
ustadi mkubwa baada ya kupokea krosi kutoka kwa Juma Abdul na kuwatoka
mabeki wa Azam kisha kupachika mpira wavuni.
Goli hilo liliwafanya Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa goli 1-0 dhidi ya Azam FC.
Kipindi cha pili Azam walirejea
kwa kasi wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara huku wakimiliki mpira
kwa dakika za katikati ya kipindi cha pili wakati Yanga kwa upande wao
walikuwa wakicheza mipira mirefu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Kipre Tchetche aliyeingia kipindi
cha pili kuchua nafasi ya Alan Wanga aliifungia Azam goli la
kusawazisha dakika ya 83 akiunganisha pasi ya Farid Musa na kuufanya
mchezo kuwa sare kwa goli 1-1.
Wakati dakika zikiwa zimeyoyoma,
Yanga walipata penati baada ya golikipa wa Azam Aishi Manula kumwangusha
mchezaji wa Yanga Simon Msuva kwenye eneo la hatari lakini Manula
alipangua penati hiyo iliyopigwa na Thabani Kamusoko.
Mwamuzi wa mchezo huo Abdallah
Kambuzi kutoka Shinyanga aliingia kwenye mgogoro na baadhi ya wachezaji
wa Azam FC ambao walikuwa wakipinga penati iliyoamriwa kupigwa
kuelekezwa kwenye lango la Azam wakidai haikua halali.
Timu hizo zilitoka sare pia
kwenye mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kagame Cup mwezi Julai
mwaka huu na Azam wakasonga mbele kwa ushindi wa mikwaju ya penati.
Timu hizo zilikutana tena kwenye
mchezo wa Ngao ya Jamii mapema mwezi Septemba mwaka ambapo dakika 90 za
mchezo huo zilimalizika kwa sare, Yanga alitwaa ubingwa huo kwa mikwaju
ya penati.
No comments
Post a Comment