Na Peter Mkwavila,Dodoma
MRADI wa usafi wa mazingira unaosimamiwa na Plan International mkoani Dodoma umefanikiwa kuwakomboa wakazi wa kijiji cha Suguta kata ya Iduo wilayani Kongwa kwa kuwapatia elimu ya kujenga vyoo vya kisasa na kuwafanya kuondokana na tabia ya kujisaidia vichakani.
Aidha elimu hiyo pia imewasaidia wakazi hao kuepukana na magonjwa ya milipuko ambayo ilikuwa ikiwatokea kila wakati.
Kauli hiyo ilisemwa na wilayani hapa na wakazi wa kijiji hicho kutokana na kunufaika na mradi huo usafi na mazingira (UMATA) ambao umetoa elimu ya kujenga vyoo bora vyenye vibuyu chirizi vya kunawia mikono.
Akizungumza mmoja wa wakazi hao,Aloyce Magomola (80) kwenye sherehe za kukabidhiwa vyeti kutokana na kila kaya kuwa na vyoo bora vya kisasa katika kijiji hicho cha Suguta.
Alisema mradi huo kabla ya kuwafikia karibu wananchi wengi walikuwa wakijisaidia vichakani,lakini mara baada ya kupatiwa elimu wameweza kuwasaidia kujenga vyoo vya kisasa.
“Kabla ya mradi kutufikia tulikuwa tunaenda kujisaidia vichakani bila kujali hata na afya zetu,ukizingatia kuwa hatukuwa na vyoo kama hivi tulivyovijenga ambavyo ni bora tena vya kisasa vikiwemo na vibuyu chirizi vya kunawia mikono”alisema Magomola
Naye Joyrose Machaku alisema kutokana na kujenga vyoo hivyo magonjwa ya milipuko katika vitongoji vya Ubungo,Ungurodi na Changombe vilivyopo katika kijiji cha Suguta yamepungua
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Charles Semsanya alisema kabla ya kuja kwa mradi huo jumla ya kaya 335 kati ya 446 ndio zilizokuwa zina vyoo bora vya kisasa na vibuyu chirizi.
“Magonjwa ya mara kwa mara ya matumbo ilikuwa ndiyo jadi katika kata hii,ukizingatia elimu ya ujenzi wa vyoo hivyo vya kisasa kulikuwa hakuna na walio wengi vichakani huko ndiko kulikuwa kama sehemu ya kujisaidia” alisema Semsanya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Plan Internation Tanzania Nyanzobe Malimi, alisema mradi huo una lengo la kuziwezesha wilaya zote za mkoa wa Dodoma kuwa na vyoo bora pamoja na kutoa elimu kuhusiana na usafi wa mazingira.
“Mradi huu mpaka sasa umefanyika katika wilaya tatu ikiwemo ya Kongwa,Chamwino na Bahi,na tumeanza na ujenzi wa vyoo vya kisasa tukiamini kuwa magonjwa mengi ya milipuko yanatoka huko,tutaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji wa mazingira’’alisema Malimi.
Imeandaliwa na John Banda
Imehaririwa na Denice J Kazenzele
january/26/2016 {jumanne}
No comments
Post a Comment