Hatimaye mshambuliaji raia wa Togo Emanuel Adebayor amepata timu ya kuichezea mara baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu sasa, tangu mwezi September mwaka jana alipoachwa na Tottenham Hotspur na kubakia kuwa huru.
Klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu soka nchini England, imemsainisha mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal mkataba wa hadi mwisho wa msimu huu kuanzia sasa.
Adebayor ambaye alitua Arsenal akitokea Monaco, alipata pia kuvichezea vilabu vya Manchester City, Tottenham Hotspur pamoja na Real Madrid alikokua kwa mkopo chini kocha Jose Mourinho.
Katika career yake ya soka nchini England, Emanuel Adebayor amepata kuzitikisa nyavu mara 94 na sasa anapata muda mwingine kuongezea idadi hiyo ya mabao na kuweza kuandika historia ya kufunga goli 100 katika ligi hiyo kwa wachezaji kutoka Afrika.
Alan Pardew kocha wa sasa wa Crystal Palace, alikua akitamani sana saini ya mshambuliaji huyo ambaye alikaribia kutua klabu ya Westham katika majira ya joto mwaka jana, na sasa huku washambuliaji wake wakiwa na idadi ndogo ya mabao (24) katika michezo 23 atanufaika na uzoefu wa Adebayor (31).
No comments
Post a Comment