Wakati mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee akilala rumande akihusishwa
na vurugu zilizotokea Jumapili wakati uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar
es Salaam ulipokwama, Mahakama ya Kisutu imelikana zuio lililotumika
kuzuia shughuli hizo.
Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 23, mwaka
huu, lakini uliahirishwa ili kuandaa mfumo bora wa upatikanaji wajumbe
kutokana na CCM kutaka kuingiza wapigakura nje ya waliotakiwa.
Ulikwama
tena Februari 8, baada ya Halmashauri ya Jiji la Dar kubaini kasoro ya
nyongeza ya majina 14 ya wajumbe kutoka manispaa za Ilala na Kinondoni.
Jumapili
iliyopita ilikuwa ni mara ya tatu, kukwama tena kutokana na zuio
lililosababishwa na kesi iliyofungiliwa na Saad Kimji na Suzan Masawe.
Hata
hivyo, zuio hilo la muda la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
lililotumika kuahirisha uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji,
uliopaswa kufanyika Februari 27, 2016 limebainika kuwa ni batili.
Jana,
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema alisema Saad
Kimji na Suzan Massawe walifungua kesi Februari 5, 2016 wakizuia
uchaguzi wa meya na naibu wake ambao ulipaswa kufanyika Februari 8,2016.
Hakimu Lema alibainisha baada ya kufungua shauri hilo, Mahakama
ya Kisutu iliweka zuio la muda ili kesi hiyo ianze kusikilizwa Februari
15, 2016 lakini walalamikaji hawakutokea mahakamani hivyo mahakama
ikapanga kusikiliza kesi hiyo Februari 23, lakini hawakutokea pia.
Alisema
kutokana na hali hiyo, aliliondoa shauri hilo mahakamani hapo na hivyo
zuio hilo likawa limekufa.
Aliongeza kuwa aliyesema Mahakama ya Kisutu
imetoa zuio ni muongo na kwamba zuio halali ni lazima liwe na jina la
Hakimu pamoja na sahihi.
Kukamatwa kwa Mdee
Katika sakata la
jana, Mdee na madiwani wengine watatu walilazwa rumande kutokana na
kutuhumiwa kumshambulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia
Mmbando
Wanatuhumiwa kufanya kosa hilo baada ya vuta nikuvute kutokea
Jumapili iliyopita wakati shughuli ya kuwasaka viongozi hao wa jiji
zilipokwaa kisiki kwa mara ya tatu, na CCM kuamua kukimbilia mahakamani.
Hali hiyo, ilizua tafrani kati ya madiwani na wananchama wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya uchaguzi
huo kuahirishwa kwa zuio la muda la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Tafrani hiyo ndiyo iliyosababisha vurugu ambazo inadaiwa kuwa katika
purukushani hizo Mdee alimshambulia Mmbando mara baada ya kutangaza
kuahirisha uchaguzi huo.
Polisi waliokuwa wanalinda usalama kwenye ukumbi wa Karimjee ambako uchaguzi huo ulitakiwa kufanyika, walimtoa nje Mmbando.
Akitoa
maelezo mafupi kwa waandishi wa habari jana baada ya Mdee kuhojiwa kwa
takriban saa sita, wakili wake , Profesa Abdalah Safari alisema mbunge
huyo anashikiliwa kwa kosa hilo na atalala rumande.
“Kimsingi
nilikuja kumsikiliza akitoa maelezo yake, ameshatoa lakini hakuna
ushahidi wowote wa kosa analodaiwa kufanya la kushambulia Theresia,”
alisema.
Hata hiyo, Profesa Safari alisema kutokana na kosa hilo Mdee
alikuwa na haki ya kuwekewa dhamana lakini polisi wamekataa.
“Mdee
angeweza kujidhamini hata mwenyewe lakini wamekataa na kutokana na kosa
hili anatakiwa kulala rumande kwa saa 48, zikizidi ina maana atapelekwa
mahakamani,” alisema.
Profesa Safari, ambaye pia ni makamu
mwenyekiti wa Chadema Bara, alisema mbali na Mdee pia madiwani watatu
wanashikiliwa na polisi kwa kosa hilo.
Madiwani hao ni Humphrey Sambo wa kata ya Mbezi, Ephraim Kinyafu (Saranga), wakati hakumtaja jina diwani wa tatu.
Awali
wakati mahojiano hayo yalipoanza saa 7:00 mchana, taarifa kutoka kwa
mmoja wa makada wa chama hicho zilieleza kuwa Mbunge wa Ukonga
(Chadema), Mwita Waitara pia alitakiwa kufika kituoni hapo kutoa maelezo
na anatarajiwa kuwasili leo.
Wakati wa polisi wakimhoji Mdee,
wanachama wa Chadema walifika kituoni hapo, akiwapo Ester Bulaya, ambaye
ni mbunge wa Bunda Mjini, Esther Matiko (Bunga Vijijini) na Henry
Kilewo ambaye ni kanda wa Chadema.
Mapema jana mchana kabla ya
Mdee kufikishwa kituoni hapo, ilielezwa kuwa polisi walizingira nyumba
yake na kumtaka aende kituoni.
Hata hivyo, mbunge huyo hakutoka hadi
alipowasiliana na wakili wake ambaye alienda naye kituoni kwa ajili ya
mahojiano.
No comments
Post a Comment