WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema atawatuma mawaziri watatu waende mkoa wa
Simiyu ili wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na wananchi ili
kubaini tatizo la mipaka baina ya wilaya hizo na Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana(Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza
na mamia ya wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya akiwa kwenye
siku ya tano ya ziara yake mkoani Simiyu.
“Tangu
niingie hapa mkoani malalamiko ya mipaka nimeyapokea kila mahali
nilikopita. Nimeamua kuwatuma mawaziri watatu ambao ni Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi; Waziri wa Maliasili
ua Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(TAMISEMI), Bw. George Simbachawene waje mkoa huu kutatua matatizo
yenu,” alisema.
“…Nitawatuma
waje na wapite kila wilaya, wakae na kuzungumza na wakulima na wafugaji
ili kubaini ni chanzo cha tatizo la migogoro hii kwenye mipaka ya
vijiji na hifadhi ya Serengeti. Pia Waziri wa TAMISEMI itabidi atoe
ufafanuzi kuhusu agizo lao la kutofanya shughuli yoyote mita 60 kutoka
kwenye mto Simiyu ili wananchi waelewe,” alisema.
Mapema,
Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira)
alimweleza waziri Mkuu mbele ya wananchi hao kwamba limetolewa zuio
linalowakata wakazi wa mkoa huo wasifanye shughuli zozote umbali wa mita
60 kutoka kwenye kingo za mto huo.
“Limebandikwa
tangazo linalokataza wananchi waishio kando ya mto Simiyu wasifanye
chochote kuanzia Julai 30, 2016. Wananchi hawajashirikishwa wala
kuelezwa chochote zaidi ya kuona bango la matangazo tu. Watu
wananakatazwa wasichote maji wala kunywesha mifugo wakati hakuna
mabwawa, itawezekanaje? Tunaomba kauli yako kuhusu jambo hili,” alisema.
Ili
kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini, Waziri Mkuu alisema
Serikali ina mpango wa kuunda mabaraza ya ardhi 100 kwa nchi nzima
ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati.
Akitoa
taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw. Erasto Sima
alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Julai mosi, 1987 ina ukubwa wa
kilometa za mraba 8,835 ambapo asilimia 49 (sawa na kilometa za mraba
4,329) ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori.
Alilitaja
eneo hilo kuwa ni pori la akiba la Maswa, sehemu ya hifadhi ya
Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na pori la hifadhi ya
usimamizi wa wanyama (WMA) la Makao na kwamba asilimia 51 iliyobakia
indiyo inayotumiwa kwa makazi ya watu, kilimo na malisho ya mifugo.
No comments
Post a Comment