Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini anatazamiwa kuwasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba hii leo, kwa shabaha ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa akishirikiana na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo.
William Ezekiel, Msemaji wa Machar amesema kiongozi huyo wa upinzani alikosa kuwasili mjini Juba jana Jumatatu kama ilivyokuwa imetarajiwa, kutokana na kile alichokitaja kuwa sababu za kilojistiki.
Amesema: "Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar amejitolea kwa dhati kupatikana amani ya kudumu nchini humo na kwamba alikosa kuwasili mjini Juba jana Jumatatu kutokana na changamoto za kilojistiki."
Jumanne iliyopita, Alfred Ladu Gore, makamu kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini aliwasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba pamoja na ujumbe wa watu 60, katika fremu ya makubaliano ya amani.
Gore na ujumbe wake waliwasili siku chache tu baada ya askari 1,370 wa waasi kuwasili mjini Juba, hatua iliyotajwa kuwa ni sehemu ya makubaliano ya amani baina ya waasi na serikali ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa hapo mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu Machar kuwa alihusika na njama ya kutaka kumuondoa madarakani.
No comments
Post a Comment